Fei Toto apiga hesabu kali Kigali

KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amefunguka mipango ya kikosi chao katika mchezo ujao dhidi ya APR ya Rwanda utakaopigwa Jumamosi.

Fei katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi alisababisha penalti iliyozaa bao pekee katika mechi hiyo baada ya kufanyiwa madhambi na beki wa APR.

Tangu atue Azam FC huu ni msimu wa pili akiwa ni kiungo mzawa mwenye mafanikio na kubeba tuzo ya mchezaji bora katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei alisema anaamini wataing’oa APR kwa kuwa walivyocheza nao kwa mara ya kwanza walijilinda sana kwa kupaki basi.

Alisema anaamini kule Kigali, wenyeji wao watafunguka na hapo ndipo Azam itapata nafasi ya kufunga zaidi kwani tayari wameshawasoma namna wanavyocheza.

“Tunakwenda kumaliza mchezo kibabe kwani tunakutana na wapinzani ambao mbinu zao tulishazisoma na tunachosubiri ni mechi ya mwisho ili wafunguke sisi tupite kushambulia. Ni wazi kuwa kwao watacheza kwa juhudi kubwa ili kuhakikisha wanatufunga na sisi tutahakikisha tunatumia kila udhaifu wao kama nafasi yetu ya kuwapiga ili tuwe na rekodi ya kumfunga kwao na ugenini,” alisema Fei.

Azam FC iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2008-2009, iliwahi kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja tu mwaka 2015 baada ya msimu wa 2013-2014 kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara.

Tangu mwaka 2014, Azam ilikuwa ikiisaka nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ikawa inajikuta ikiangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

Hivyo itashuka katika mchezo wa marudiano dhidi ya APR, ikiwa na rekodi ya kuwafunga bao 1-0.

Related Posts