Gamondi ashtukia mchongo, afanya maamuzi ‘KONKI’

YANGA ina uhakika mkubwa wa kuimaliza mechi ya marudiano dhidi ya Vital’O ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa Jumamosi baada ya ushindi mabao 4-0 wikiendi iliyopita.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi mwili wake upo Dar es Salaam lakini akili ipo Addis Ababa, Ethiopia kwenye mechi ya marudiano ya CBE ya huko na SC Villa ya Uganda. Mshindi wa mechi hiyo atacheza na Yanga ambayo inahitaji japo sare yoyote kusonga mbele. Villa ililala mabao 1-2 nyumbani.

Endapo Yanga itafuzu na kukutana na mshindi kati ya CBE au Vila, mabingwa hao wa soka Tanzania wataanzia ugenini kati ya Septemba 13-15 kisha kurudiana hapa nchini kati ya Septemba 20-22.

Gamondi ameangalia rekodi za Yanga dhidi ya timu za Ethiopia akaamua kujiongeza na kutuma watu haraka ambao wikiendi hii watakuwa jukwaani wakiangalia mechi hiyo.

Rekodi zinaonyesha kwamba kwenye michuano ya CAF Yanga haijawahi kushinda nchini Ethiopia.

Kati ya Kocha wao msaidizi Mussa Nd’ew au mtaalam wa kuwasoma wapinzani Msauz Mpho Maruping, mmoja wao ataongoza msafara wa watu wawili kwenye kuisoma CBE ambao taarifa zao za awali imepenyezewa kwamba jamaa wanacheza soka la pasi nyingi na kasi hatua ambayo wanataka kuwajua zaidi haraka kabla ya kukutana nao.

CBE ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchukua ubingwa wa kwao kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe 1982.

Timu hiyo imeshiriki mara mbili mashindano ya Afrika ambapo mara mbili ikicheza Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa hatua ya mtoano miaka ya 2005 na 2010 kabla ya msimu huu kuja kutanua historia yao kwa kucheza ligi ya mabingwa.

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi ingawa hakutaka sana kuwazungumzia wapinzani hao akidai bado anataka kumalizana kwanza na Vital’O lakini Mwanaaspoti linafahamu ameshawaachia mabosi wake mahitaji ya kutaka kuwajua wapinzani wao.

Mbali na safari hiyo pia Yanga ina mkanda wa video wa mechi ya kwanza kati ya Villa na CBE ambao Waganda hao walijikuta wakikubali kipigo hicho kisha baadaye kucheza pungufu kufuatia mchezaji wao mmoja kupewa kadi nyekundu dakika za mwisho za mchezo.

“Tunataka kuhakikisha kila kitu tunakinasa mapema, hatutaki kuidharau timu yoyote ndio maana unaona tunapambana kuhakikisha tunatuma watu huko Ethiopia na hapa ni safari ya masaa matano tu,”alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

YANGA HAIJASHINDA ETHIOPIA

Yanga dhidi ya timu za Ethiopia katika michuano ya CAF ina rekodi ya kuzitoa mara tatu kati ya nne walizokutana huku yenyewe ikitolewa mara mmoja hatua ya mtoano.

Yanga mbali ya kuzitoa timu hizo za Ethiopia lakini inajivunia rekodi yake ya kufunga mabao mengi wanapocheza na Wahabeshi hao.

Hata hivyo pamoja na Yanga kuzionea timu za Ethiopia bado mabingwa hao wa kihistoria Tanzania hawajawahi kushinda Ethiopia wakitoka sare mbili na kufungwa mbili wanapocheza ugenini.

Yanga ilikutana kwa mara ya kwanza klabu ya Ethiopia mwaka 1969, katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika sasa Ligi ya Mabingwa Yanga ilitoa Saint-George ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 5-0.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia timu hizo zilitoka suluhu na mechi ya marudiano Yanga ilishinda 5-0 na kusonga mbele hadi robo fainali.

Kisha Yanga ilikutana na Coffee FC ya Ethiopia mwaka 1998 na kuitoa kwa jumla ya mabao 3-8, katika hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Ethiopia Coffee FC ililazimisha sare 2-2 katika mchezo wa marudiano Yanga ilishinda 1–6 nyumbani na kufanikiwa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Katika Kombe la Shirikisho mwaka 2011, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-4, ilianzia nyumbani na kulazimishwa sare 4-4 na Dedebit kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Ethiopia wenyeji, Dedebit walichapa Yanga mabao 2-0.

Mwaka 2018, ilicheza dhidi ya Welaita Dicha katika Kombe la Shirikisho na kufuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 2-1. Mchezo wa kwanza nyumbani Yanga ilishinda 2-0, ilipoenda ugenini ikafungwa 1-0.

1969  Yanga        5-0 St. George

1969   St. George 0-0    Yanga

1998  Coffee FC  2-2    Yanga

1998  Yanga                  6-1    Coffee                 

2024    CBE   vs Yanga?

2011           Yanga                  4-4    Dedebit              

2011           Dedebit               2-0    Yanga                 

2018           Yanga                  2-0    Welaita Dicha    

2018           Welaita Dicha     1-0    Yanga                 

Related Posts