WACHEZA gofu 70 kutoka mataifa tisa duniani wanategemewa kunogesha msimu wa utalii Zanzibar huku viwanja vya gofu vya Sea Cliff vikiwa tayari kwa ajili mashindano ya watendaji wakuu na maofisa wa kibalozi kutoka nchi mbalimbali mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Elias Soka, nahodha ya klabu ya Sea Cliff na mratibu wa mashindano hayo kila mwaka, Septemba 2, mwaka huu ndiyo siku ya mwisho ya kujiandikisha ikiwa ni ya tano kabla ya mashindano kuanza Septemba 7, mwaka huu. .
Soka alisema wachezaji 70 ndiyo wanatakiwa kushiriki mashindano mwaka huu.
Mashindano hayo siku moja yatapigwa katika mashimo 18 ya viwanja vya Sea Cliff vilivyopo katika fukwe za Mangapwani, Zanzibar.
Alisema mashindano hayo ambayo hujulikana kama Faraja ya Burudani kwa Maofisa Watendaji Wakuu wa kampuni na taasisi pamoja na maofisa kutoka balozi mbalimbali zilipo ndani na nje ya nchi, ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii Zanzibar na ndiyo maana huvuta ushiriki wa watu wengi.
“Mashindano haya ni sehemu ya kampeni ya Tanzania kuboresha utalii kwa kutumia michezo kama gofu,” alisema mratibu huyo.
Miongoni mwa vivutio vikubwa kwa wachezaji ni zawadi na hii inachangiwa na uwepo wa wadhamini wengi.
“Kumekuwepo na ongezeko kubwa la wadhamini hali ambayo itasaidia pia kuboresha ukubwa wa zawadi za washindi watakaoshinda michuano hii,” alisema.
“Hii itasaidia pia kuvitangaza viwanja vya Sea Cliff kama moja ya viwanja bora vya mashimo tisa vilivyopo kando ya Bahari ya Hindi.”
Mashindano hayo hufanyika kila mwaka Zanzibar na washiriki wake wengi hutoka pembe zote za Afrika na nje ya bara hilo, kwa mujibu wa Soka.