Dodoma. ‘Serikali za mitaa, sauti ya wananchi, jitokezeni kushiriki uchaguzi.’ Kauli hii inahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, mwaka huu.
Kwa kushiriki uchaguzi, wananchi wanapata fursa ya kuchagua viongozi wanaowaamini watawakilisha sauti zao kwa ufanisi.
Ushiriki huu unahakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika na kujumuishwa katika maamuzi yanayowagusa moja kwa moja, kama vile mipango ya maendeleo na huduma za kijamii.
Kwa hiyo, kauli hii ni mwito wa kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi ili kuhakikisha wanapata uwakilishi unaowakilisha masilahi yao kwa usahihi na haki.
Kuhakikisha sauti za wananchi zinakuwa madhubuti na zinasikika Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa tayari ametoa kanuni za uchaguzi ikiwamo kuainisha mambo yanayoweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni masuala yanayoweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi au utekelezaji wa shughuli yoyote ya uchaguzi ni kutokuwepo kwa mgombea au wakala wa mgombea wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura au kutangaza matokeo.
Mbali na hayo ni mgombea au wakala wa mgombea kukataa kusaini fomu ya matokeo.
Mgombea yeyote ambaye hakuridhika na matokeo ya uchaguzi au uendeshaji wa uchaguzi anaweza kufungua shauri katika Mahakama ya Wilaya ndani ya siku 30 tangu siku ya kutangaza matokeo ya uchaguzi.
Msimamizi wa uchaguzi atahakikisha anatunza kwa usalama nyaraka zote zinazohusu uendeshaji wa uchaguzi.
“Msimamizi wa uchaguzi atahakikisha nyaraka zote zinazohusu uendeshaji wa uchaguzi zinateketezwa baada ya kupita kipindi cha siku 30 toka siku ya uchaguzi isipokuwa kama itaelekezwa vinginevyo kwa amri ya Mahakama.
Kanuni zinaelekeza kuwa nafasi ya uenyekiti au ujumbe itakuwa wazi endapo kutatokea kifo cha mwenyekiti au mjumbe, mwenyekiti au mjumbe kujiuzulu wadhifa wake, mwenyekiti au mjumbe kukosa sifa za kuwa mgombea, na kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Sababu zingine ni mwenyekiti au mjumbe kukoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini, mwenyekiti au mjumbe kuhama eneo alilochaguliwa kushika uongozi, mwenyekiti kutoitisha mikutano mitatu ya kawaida mfululizo bila kuwa na sababu za msingi.
Kanuni zinataja sababu zingine ni mwenyekiti au mjumbe kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya kawaida bila kuwa na sababu ya msingi, kugawanywa kwa kijiji au kitongoji au mtaa na mwenyekiti au mjumbe kuvuliwa madaraka kwa mujibu wa sheria.
Kanuni zinataja kuwa mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo, ataharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusu uchaguzi.
Makosa mengine ni endapo atatoa taarifa za uongo ili aweze kupiga kura au kugombea nafasi ya uenyekiti au ujumbe, kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye orodha ya wapigakura, kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja.
Kwa mujibu wa kanuni makosa mengine ni endapo atatishia wapigakura au wagombea ili kuvuruga uchaguzi, atafanya kampeni siku ya uchaguzi, ataonyesha ishara au kuvaa mavazi yanayoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa katika eneo la mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.
Lingine ni endapo atamzuia msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, mjumbe wa kamati ya rufani au mtumishi wa umma aliyeteuliwa kusimamia uchaguzi kutekeleza majukumu yake.
Makosa mengine ni endapo atakiuka masharti ya kiapo chake, atapatikana na karatasi za kupigia kura zaidi ya moja kwa nafasi moja inayogombewa, atavuruga ratiba ya mikutano ya kampeni za uchaguzi au atavunja masharti ya kampeni za uchaguzi, atafanya jambo lolote kinyume cha kanuni hizi.
Makosa mengine ni endapo atakutwa na silaha kwenye eneo la uteuzi wa wagombea, mikutano ya kampeni, eneo la usikilizaji wa rufaa, kituo cha kuandikisha wapiga kura au kituo cha kupigia na kuhesabu kura.
Mbali ya hayo, ni endapo mtu atatangaza matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi au msimamizi wa kituo kwa mujibu wa kanuni hizi.
Mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote chini ya kanuni ndogo ya (1) atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja, yaani faini na kifungo.
Pia, mtu yeyote atakayetumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayoashiria unyanyasaji na ukatilii wa kijinsia katika uchaguzi
atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia ataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za maadili.
Kanuni zinaelekeza kutakuwa na kinga kwa msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, wajumbe wa kamati ya rufani au mtumishi yeyote wa umma.
Kinga hiyo inaeleza wote hao waliohusika na usimamizi wa uchaguzi hatawajibika kwa jinai au madai au kuchukuliwa hatua za kinidhamu au kiutawala kwa jambo lolote alilolifanya au kuacha kufanya kwa nia njema wakati wa kutekeleza majukumu yao.