Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam imepanga kutoa hukumu ya kesi ya mkopo inayozikabili Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK), Oktoba 18, 2024.
Mahakama imepanga kutoa hukumu tarehe hiyo baada ya kumaliza kusikiliza ushahidi wa pande zote.
Usikilizwaji wa kesi hiyo imefungwa rasmi leo, Jumatano, Agosti 21, 2024, baada ya shahidi wa tatu wa upande wa utetezi wakili Thomas Mihayo Sipemba kumaliza kutoa ushahidi wake.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Agatho Ubena, imefunguliwa na kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kahama Import & Export Commercial Agency Limited, zinazodaiwa kukopeshwa pesa na benki hizo.
Wadai wengine katika kesi hiyo namba 78 ya mwaka 2023 ni wadhamini wa mkopo unaobishaniwa; Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.
Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo baada ya kuandikiwa barua na benki hizo zikiwataka kulipa Dola za Marekani 46,658,395.81 (zaidi ya Sh122.54 bilioni).
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, kampuni hizo zinadai hazijawahi kupokea mkopo wa Dola 32 milioni kutoka kwa wadaiwa katika kesi hiyo, huku wakidai benki hizo zilitoa mkopo huo kwa Kampuni ya Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya.
Badala yake zinadai zenyewe zilipokea mkopo wa Dola 30 milioni kutoka kwa Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya, ambapo tayari zilishaanza kulipa sehemu ya mkopo huo.
Benki hizo nazo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo zikisisitiza kuzikopesha mkopo ambao hazikuurejesha, huku zilipinga na kuzitaka zithibitishe kuwepo kwa kampuni inayoitwa Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya, ambayo kampuni hizo zinadai kuwa ndio ilikopeshwa na benki hizo.
Kwa mujibu wa benki hizo kwa sasa deni hilo limefikia Dola za Marekani 47,228592.53. (zaidi ya Sh123 milioni) kiasi kinachojumuisha deni la msingi la mkopo wa Dola 32 milioni, riba na faini.
Katika ushahidi wake shahidi huyo wa mwisho wa upande wa utetezi ameieleza mahakama hiyo kuwa yeye ndiye aliyesimamia mchakato wa uhamishaji wa hati za mali za wadai (wakopaji) zilizokuwa katika Benki ya CRDB kwenda Equity Bank.
Kwa mujibu wa shahidi huyo hati za mali hizo zilihamishwa kutoka CRDB na kwenda Equity Bank, baada ya benki hizo kutoa fedha za mkopo ulioombwa na kampuni hizo, ambazo sehemu yake zilitumika kulipia madeni zilizokuwa zikidaiwa na Benki ya CRDB.
Hivyo hati za mali hizo zilihamishiwa Equity Bank na kusajiliwa huko kwa ajili ya kudhamini mkopo huo.
Baada ya maelezo hayo mafupi ya shahidi huyo akiongozwa na wakili wa benki hizo, Zaharani Sinare, kufafanua maelezo ya ushahidi wake wa maandishi aliokwishauwasilisha mahakamani, Wakili wa wadai katika kesi hiyo kampuni za Kahama na wenzake), Frank Mwalongo hakuwa na swali la dodoso.
Hivyo wakili Sinare ameieleza Mahakama kuwa hawatakuwa na shahidi mwingine, hivyo wadaiwa (wakopeshaji, benki) wanafunga ushahidi wao.
Baada ya taarifa hiyo ndipo Jaji Ubena akapanga kutoa hukumu Oktoba 18, 2024.