Tehran. Iran imefunga kituo cha lugha kinachomilikiwa na ubalozi wa Ujerumani, huku sababu ikitajwa kuwa ni kufungwa kwa vituo vya dini ya Kiislamu nchini Ujerumani.
Mahakama ya Iran imefunga ofisi mbili za taasisi hiyo, ikizitaja kama vituo haramu vyenye uhusiano na Serikali ya Ujerumani, ambayo imekiuka sheria za Iran na kufanya vitendo vingi haramu.
Tovuti ya AP imeripoti kuwa, “Irani Jumanne Agosti 20, 2024 ilifunga taasisi ya mwisho ya lugha iliyoidhinishwa na ubalozi wa Ujerumani, vyombo vya habari vya ndani vilisema kuwa hatua hiyo ni kulipiza kisasi kwa kufungwa kwa vituo vya Kiislamu katika nchi za Ulaya.”
Nayo tovuti ya Nournews.ir ya nchini Iran inayoaminika kuwa karibu na vyombo vya usalama, ilichapisha picha ya vikosi vya polisi vikishusha alama ya jina la taasisi hiyo.
Taasisi ya kufundisha lugha ya kijerumani ilianzishwa katika mji mkuu wa Iran mwaka wa 1995, kulingana na taarifa ya ubalozi wa Ujerumani.
Kufungwa kwake kunakuja baada ya mamlaka ya Ujerumani kukifunga Kituo cha Kiislamu cha Hamburg, na mashirika madogo matano, Julai, 2024 yakikishutumu kuwa kinaunga mkono kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah.