Jubilee yaipiga tafu Don Bosco

KATIKA kuendeleza vipaji vya wachezaji wa mchezo wa kikapu nchini, Bima ya Maisha ya Jubilee imeingia katika udhamini wa timu ya Don Bosco Oysterbay yenye wachezaji 60 wa rika mbalimbali kupitia mchezo wa mpira wa kikapu.

Akizungumza leo wakati wa kukabidhi vifaa, Mkurugenzi Mkuu wa Bima ya Maisha ya Jubilee, Helena Mzena, amesema kauli mbiu ya Ishi Huru imewasukuma kuidhamini timu ya Don Bosco.

“Tumeamua kuidhamini hii timu kwa sababu tunajua ni moja ya timu inayosaidia vijana wa rika mbalimbali katika kutimiza malengo na ndoto zao kwa njia ya michezo, hivyo tumeona ni jambo zuri ambalo tunaweza kushirikiana katika kurudisha kwa jamii,” alisema Helena.

Alisema kwa kuanzia wametoa vifaa ambavyo ni boksi la huduma ya kwanza, jezi na mipira huku akibainisha kwamba watashiriki kwenye mechi tano zitakazochezwa na timu hiyo ili kuwatia moyo na kuwapa hamasa katika kuongeza juhudi.

Mlezi wa Kituo cha Michezo cha Don Bosco Oysterbay, Padri Joachim Sivali, alisema kwao ni faraja kupata wadhamini ambao wanajali michezo na kusaidia ukuaji wa vipaji kwa vijana.

“Vijana huwa wanafurahi wakiona kuna watu wanawaunga mkono na kuona umuhimu wa michezo yao na hii inawafanya waendelee kujituma zaidi na kufanya vizuri,” alisema Padri Sivali.

Padri huyo alisema kuna taasisi chache zinazojitolea kudhamini michezo hivyo wanapojitokeza wanaounga mkono wapewe ushirikiano.

Related Posts