KESI ‘WALIOTUMWA NA AFANDE’: Mashahidi kuendelea kusikilizwa leo, watuhumiwa wafika mahakamani

Dodoma. Leo ni siku ya tatu tangu watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti wa binti wa Yombo Dovya jijini Dar es salaam wafikishwe mahakamani na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Kesi hiyo itaendelea leo Agosti 21, 2024 kwa kuwasikiliza mashahidi ambao wameletwa na upande wa Jamhuri.

Kesi hiyo namba 23476 ya mwaka 2024 iliahirishwa jana kutokana na muda kuisha ambapo kati ya mashahidi watano walioletwa na Jamhuri walimsikiliza shahidi mmoja, ambaye hata hivyo hawakupata muda wa kumuhoji na wataendelea kusikiliza ushahidi wake leo.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea wanne wakiongozwa na Godfrey Wasonga, Meshaki Ngamando, Boniventura Njeru na Sadick Omari Sadick huku upande wa Jamhuri ukiwasilishwa na mawakili watatu.

Watuhumiwa hao wameshafika mahakamani kutokea magereza ambapo kesi yao itaanza kusikilizwa muda wowote kwenye chemba ya mahakama, ambapo watu wengine hawaruhusiwi kuingia isipokuwa mawakili na washtakiwa kutokana na unyeti wa kesi hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude amesema kinachoendelea kwa sasa ni kutoa ushahidi ambapo majina ya mashahidi yamefichwa ili kutoharibu mwenendo wa kesi.

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi

Related Posts