Kituo cha afya Lupalilo chapokea kitanda kupunguza changamoto ya upungufu wa vifaa tiba

Katika kupunguza changamoto ya vifaa tiba kwenye majengo mapya ya kituo cha afya Lupalilo kilichopo wilaya ya Makete mkoani Njombe,mganga mkuu wa halmashauri hiyo amepokea kitanda chenye thamani ya takribani Milioni 2.5 kwa ajili ya wagonjwa kituoni hapo.

Akizungumza baada ya kupokea kitanda hicho mbele ya wananchi wa Lupalilo kilichotolewa na mwenyekiti wa UWT mkoa wa Njombe Dkt.Scolastika Kevela,Mganga mkuu Dkt.Ligobert Kalisa amesema msaada huo unakwenda kuongeza ufanisi wa huduma kwa wagonjwa kwa kuwa bado kituo hicho cha afya kinakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba.

Vile vile amesema halmashauri hiyo inatekeleza takribani miradi mipya mitano ikiwemo kituo hicho ambapo majengo mapya matano yenye thamani takribani milioni mia tano na hamsini yameanza kutumika na wataendelea kupokea vifaa vya takribani milioni mia tatu ili kurahisisha wananchi kupata huduma kwenye vituo vya serikali

“Kitanda hiki kina uwezo wa kwenda mpaka milioni mbili na nusu kwa hiyo idara ya afya tunashukuru sana kwa masaada huu ambao umetuongezea katika misaada ile ambayo imekuja ili kuhakikisha wateja wetu wanaokuja katika kituo hiki wanapata huduma stahiki,kwasababu kama usingeleta wewe ingetubidi tuanze kutafuta mapato yetu ya ndani au ya kituo ili tuweze kununua kitanda hiki”Amesema Dkt.Kalisa.

Dkt.Scolastika Kevela ni mwenyekiti wa UWT mkoa wa Njombe amesema ametoa mchango huo ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha afya za watanzania.

“Nimeleta zawadi hii ili iweze kuwafaa wenzangu kwenye kituo cha afya cha Lupalilo kumuunga mkono Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi anazozifanya kwenye afya kwa vitendo”

Kwa niaba ya wananchi wa kata ya Lupalilo diwani wa kata hiyo Iman Mahenge ameshukuru kwa msaada huo kwa kuwa jambo hilo limekwenda kugusa mioyo ya wakazi wa Lupalilo.

Related Posts