Licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutengua hukumu yake iliyobatilisha Katiba ya Klabu ya Dar es Salaam, Young African Sports, maarufu kama Yanga, ya mwaka 2011, kufuatia kesi iliyofunguliwa na Juma Ally Magoma na Geoffrey Mwaipopo, pande hizo mbili zinaendelea kukabana koo mahakamani.
Hii inatokana na hatua ya Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga kuwawekea kigingi cha pingamizi la hoja za kisheria Magoma na mwenzake katika rufaa yao waliyoikata Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, linalolenga kuishawishi Mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo bila kuisikiliza.
Katika rufaa hiyo, Magoma na Mwaipopo ambao wanawakilishwa na Wakili Jacob Mashenene wanapinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ulioiruhusu Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga kufungua shauri la maombi ya marejeo ya hukumu yake ( Mahakama hiyo).
Magoma na mwenzake wamekata rufaa hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga, ambayo ndio mjibu rufaa wa kwanza.
Wajibu rufaa wengine ni waliowahi kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo, Fatma Abeid Karume ( bado mjumbe mpaka sasa), Abeid Abeid na Jabiri Katundu (mjibu rufaa wa pili, wa tatu na wa nne mtawalia)
Wamekata rufaa hiyo wakipinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kwa madai kuwa iliwapa wadhamini hao wa Yanga ruhusa ya kufungua maombi hayo ya marejeo ya hukumu hiyo bila wao kupewa nafasi ya kusikilizwa katika maombi hayo ya Yanga.
Sababu nyingine wanadai kuwa mahakama hiyo ya Kisutu iliwakubalia wadhamini hao wa Yanga kufungua shauri hilo la maombi ya marejeo ya hukumu hiyo, bila kutoa sababu za msingi na hati ya kiapo kilichounga mkono maombi ya marejeo kuwa na kasoro za kisheria.
Rufaa hiyo inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Salma Maghimbi imetajwa leo Jumatano, Agosti 21 2024 kwa ajili ya kuangalia kama warufani ( kina Magoma) wamshatekeleza amri ya Mahakama..
Amri hiyo ni kuwapelekea nyaraka za kesi hiyo wajibu rufaa wa pili (Fatma) na WA nne (Katundu), ambao wakati rufaa hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza walikuwa bado hawajapewa nyaraka hizo na warufani.
Wakizungumza na waandishi baada ya rufaa hiyo kuahirishwa, mawakili wa pande zote, Kalaghe Rashid wa wajibu rufaa (Yanga) na Mashenene wamesema kuwa wajibu rufaa wamewasilisha pingamizi la awali na kwamba Mahakama imepanga kusikiliza pingamizi hilo Ijumaa Agosti 30, 2024 saa 2:00 asubuhi.
Wakili Rashid amesema kuwa katika pingamizi hilo wameibua hoja tatu, kwanza ikiwa wakidai kuwa uamuzi ambao kina Magoma wameukatia rufaa ni uamuzi mdogo ambao kisheria haiwezi kukatiwa rufaa.
Pia Wakili Rashid amedai kuwa rufaa hiyo imeshapitwa na tukio kwa kuwa tayari Mahakama ya Kisutu imeshasikiliza maombi yao ya marejeo na kutengua hukumu yake ya awali na kwamba kwa hiyo hakuna chochote kinachoweza kubadikishwa hata kama rufaa yao ikikubaliwa.
Agosti 4, 2022 Magoma na mwenzake Mwaipopo, wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo walifungua kesi wakipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.
Hivyo waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa Katiba ya mwaka 2011 ni batili na wajumbe wa Bodi waliopo kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.
Kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo kwa madai kuwa walipelekewa wito wa Mahakama lakini hawakuitikia.
Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Pamela Mazengo, Agosti 2, 2023, mahakama hiyo ilibatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.
Mahakama hiyo ilikubalina na madai na maombi ya kina Magoma, ikatamka kuwa Katiba ya sasa ya Yanga, (2011) haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968.
Hivyo ilisema kuwa Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika ( mwenyekiti ), Fatma Abeid Aman Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.
Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batil.
Hata hivyo hukumu hiyo haikuwahi kujulikana hadi Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaya ilipoibuka katika vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani hapo kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.
Uongozi wa Klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wake wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza kuwa hakuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo, huku akibainisha kuwa klabu hiyo itavhukua hatua za kuupinga, Kwa kuwa haikukubaliana nao.
Mpaka wakati huo ilipoupata uamuzi huo ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.
Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga uamuzi huo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.
Kufuatia uamuzi huo ndipo kina Magoma wakakata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.
Kabla ya rufaa hiyo ya kina Magoma haijaanza kusikilizwa, Agosti 5, 2024, Mahakama ya Kisutu ilisikilizwa shauri la maombi ya marejeo la Wadhamini wa Yanga, ambapo pande zote wakiwemo kina Magoma kupitia Wakili wao Mashenene waliaikilizwa.
Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa Agosti 9, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga ilikubaliana na hoja za Yanga na kutengua hukumu yake ya awali ambayo ilikuwa imebatilisha Katiba ya sasa ya klabu hiyo.