Makambo, Yacouba wakomaliwa Tabora Utd

KIKOSI cha Tabora United kimerejea jana mazoezini baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa mabao 3-0 mbele ya Simba, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya Francis Kimanzi akiwakomalia nyota wapya akiwemo Heritier Makambo na Yacouba Songne waliokosa mchezo uliopita.

Baada ya kichapo hicho, Kimanzi alitoa mapumziko ya siku mbili kwa mastaa wote waliocheza mchezo huo na Simba, huku kwa Makambo na wengine wa kigeni ambao hawakucheza wakipewa programu za mazoezi peke yao hadi jana walipoungana na wenzao.

Katika mazoezi hayo walishuhudiwa nyota wapya wakiwemo Heritier Makambo na Yacouba Songne waliowahi kutamba na Yanga hapa nchini, sambamba na aliyekuwa kiungo wa Singida Black Stars raia wa Nigeria, Morice Chukwu na Mkongomani, Heritier Munani kutokea FC Lupopo.

Nyota wengine ni kipa, Victor Sochima, beki wa kulia, Enyinnaya Kazie Godswill na kiungo mshambuliaji, Shedrack Asiegbu ambao wote wamejiunga na kikosi hicho cha mkoani Tabora msimu huu baada ya kuachana na Rivers United FC ya kwao Nigeria.

Licha ya ubora wa nyota hao, mshambuliaji anayesubiriwa kwa hamu zaidi ni Mkongomani Makambo ambaye amerudi tena nchini kwa mara ya tatu baada ya kuichezea Yanga misimu tofauti na kuteka mashabiki na aina yake ya ushangiliaji ya kuwajaza.

Kwa mara ya kwanza Makambo alitua nchini Julai Mosi, 2018 akitokea FC Lupopo ya  DR Congo na kuitumikia hadi Agosti 10, 2019 na kujiunga na AC Horoya ya Guinea na kuichezea kwa misimu miwili kisha kurejea tena Yanga na kuondoka Januari 2023.

Makambo amejiunga na Tabora msimu huu baada ya kuachana na Al Murooj ya Libya huku msimu bora kwake ukiwa ni ule wa kwanza akiwa na Yanga alipofunga mabao 21 katika mashindano mbalimbali.

Katika mabao hayo 21, Makambo alifunga 17 ya Ligi Kuu Bara, manne katika Kombe la Shirikisho la FA akizidiwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kutupia kambani mabao 23.

Kocha Mkuu wa Tabora United, Francis Kimanzi alisema, sababu kubwa ya kutowapa mapumziko wachezaji hao ni kutokana na kutokuwa na michezo ya kiushindani kama wenzao, ingawa ameridhika na uwezo wao ambao wameuonyesha hadi sasa mazoezini.

“Natumaini hadi kufikia mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya Namungo watakuwa wako fiti kwa asilimia kubwa, ilikuwa pigo sana kwetu kuwakosa na Simba ingawa hatuwezi kujutia,” alisema.

Related Posts