Matampi, Lawi waitesa coastal | Mwanaspoti

KUNA uhusiano mkubwa wa kuanza kufanya vibaya msimu huu kwa safu ya ulinzi ya Coastal Union na kukosekana uwanjani kwa kipa tegemeo, Ley Matampi na beki wa kati, Lameck Lawi.

Tofauti na msimu uliopita ambao Coastal Union ilikuwa miongoni mwa timu zenye safu imara za ulinzi, mambo yameonekana kwenda kinyume msimu huu ambapo imeonyesha udhaifu mkubwa katika ukuta wake kabla hata msimu haujaanza kuchangamka.

Udhaifu huo unaonekana kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa Matampi ambaye inaripotiwa kwamba kocha David Ouma ameamua kutompa nafasi kutokana na mchezaji huyo kuchelewa kuungana na wenzake wakati wa maandalizi ya msimu pamoja na beki Lameck Lawi ambaye anafanya majaribio AIK Fotboll ya Sweden.

Msimu uliopita, katika mechi 30 za ligi, Coastal Union huku ikiwa na Matampi na Lawi katika idadi kubwa ya michezo, iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19 tu katika mechi 30 za Ligi Kuu ikiwa ni wastani wa bao 0.6 kwa mechi.

Lakini katika hali ya kushangaza, katika mechi sita za mashindano ambazo Coastal Union imecheza hivi karibuni kabla hata ya kucheza Ligi Kuu msimu huu, timu hiyo imesharuhusu nyavu zake kutikiswa mara 12, ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mechi.

Pengo la Matampi na Lawi lilianza kuonekana katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambapo katika mechi tatu ambazo Coastal Union ilicheza dhidi ya Dekedaha (Somalia), Al Wadi (Sudan) na JKU (Zanzibar) iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.

Ilianza kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dekedaha, ikapoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya JKU na mechi ya tatu ikatoka sare ya bao 1-1 na Al Wadi.

Katika mechi hizo tatu, Coastal Union ilimtumia kipa Athuman Msekeni na kwenye benchi alikuwepo Chuma Ramadhani.

Baada ya hapo, udhaifu wa safu ya ulinzi ya Coastal Union uliendelea kwenye mashindano ya Ngao ya Jamii ambapo katika mechi mbili ilizocheza iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, ikifungwa mabao 5-2 na Azam FC kwenye nusu fainali na ikafungwa bao 1-0 na Simba katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu.

Dhidi ya Azam, kipa aliyekuwa langoni alikuwa ni Athuman Msekeni na mchezo uliofuata dhidi ya Simba, Coastal Union ilimtumia kipa Chuma Ramadhan.

Pengo la Matampi likaonekana tena Jumamosi iliyopita katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo Coastal Union ilicheza ugenini dhidi ya Onze Bravos ya huko Angola ambapo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu langoni akiwepo Chuma.

Ikumbukwe Matampi ndiye aliibuka mshindi wa Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuongoza kwa kucheza idadi kubwa ya michezo bila kuruhusu bao akifanya hivyo mara 15.

Ukiachana na eneo la kipa, wakati Lawi amekosekana ndani ya Coastal Union, eneo la beki wa kati wamekuwa wakibadilishwa mabeki mara kwa mara katika mechi hizo ambapo waliotumika wapo Anguti Luis na Mukrim Issa.

Kocha wa Coastal Union, David Ouma alisema kuwa anaamini safu yake ya ulinzi itakaa sawa na kuruhusu mabao mengi hakutokani na kumkosa mchezaji fulani.

“Wachezaji wote wa Coastal ni muhimu na mabao tunayoruhusu yanatokana na makosa ya kitimu kwani ukiyaangalia ni mepesi lakini kama ambavyo nilisema kuwa timu ina wachezaji wengi wapya na wanahitaji muda kuzoeana.

“Silaha kubwa ya Coastal Union ni safu imara ya ulinzi ambayo imekuwa hairuhusu mabao kirahisi hivyo tutarudi katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi hayo mapungufu na tutakuwa vizuri,” alisema Ouma.

Kipa wa zamani wa Coastal Union, Hussein Shariff ‘Casillas’ alisema anaamini timu hiyo itakaa sawa katika safu ya ulinzi.

“Matampi ni kipa mzoefu kulinganisha na hao wengine waliopo hivyo uwepo wake langoni unakuwa na msaada mkubwa lakini hata yeye alipata uzoefu kwa sababu ya kucheza hivyo ninaamini hao makipa wengine kadiri wanavyocheza ndio wanapata uzoefu.

“Kingine ambacho Coastal wanatakiwa washukuru ni kwamba tatizo limeonekana mapema hivyo benchi la ufundi litapata nafasi ya kulirekebisha. Ingekuwa hatari zaidi iwapo udhaifu huo ungejitokeza wakati ligi inaendelea,” alisema Casillas.

Coastal Union inatarajia kurudiana na Onze Bravos, Jumapili saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar ambapo inahitajika kupata ushindi wa kuanzia mabao 4-0 ili iweze kusonga mbele.

Related Posts