Mousa Camara amtisha Diarra, Matampi

KIPA mpya wa Simba, Mousa Camara ameweka wazi malengo yake msimu huu na kutangaza vita dhidi ya Djigui Diarra wa Yanga na Lay Matampi kutoka Coastal Union.

Camara ambaye ametua Simba msimu huu akitokea Horoya AC ya Guinea na ndiye kipa aliyedaka mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Tabora United akitoka bila ya kuruhusu nyavu kutikiswa ikiwa ina maana kuwa tayari ana Clean Sheet ya kwanza.

Nyota huyo amekuwa na rekodi ya kuchukua Tuzo ya Kipa Bora mara mbili kwenye Ligi ya Guinea akiwa na Horoya, akiisaidia timu hiyo kuchukua  mataji manne ya Ligi, FA (3) na Super Cup (2).

Uwepo wa Camara akiwa kipa namba moja kwa sasa, unamaanisha kuwa timu tatu kubwa ndani ya ligi, Simba, Yanga na Azam zina makipa namba moja kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti Camara ambaye anatajwa kuwa mmoja wa makipa wa kisasa kutokana na uwezo wake wa juu wa kutumia miguu, alisema msimu huu anataka kuwa ndani ya makipa watatu bora kwenye Ligi ya Tanzania kwa kuwa anaamini kuhusu uwezo wake.

Aidha alieleza kuwa, anatambua kwenye ligi kuna makipa wengi bora akiwemo Diarra ambaye anamjua tangu akiwa kwao Guinea huku Matampi akimjua kwa mbali na ili awe bora ni lazima apambane na wazoefu hao kwenye ligi.

“Diarra, Matampi wote ni makipa wazuri lakini nataka kuwa na mwanzo mzuri ndani ya kikosi cha Simba na kuwa miongoni mwa makipa watakaokuwa wakiongoza kwenye chati Ligi Kuu Bara.

“Malengo yangu haya yanatokana na ubora wa kikosi chetu licha ya kwamba ni kipya, lakini naamini kadiri tunavyoendelea kuzoeana tutakuwa na timu nzuri huko mbele,” alisema Camara.

Kipa huyo ambaye alisajiliwa na Simba baada ya uongozi wa timu hiyo kutoa taarifa za kuumia aliyekuwa kipa namba moja kikosini hapo, Ayoub Lakred, alisema: “Ukuta wetu nao ni sababu ya pili ambayo inanipa imani kwamba nitaweza kufikia malengo yangu ndani ya ligi na kikosi kwa ujumla kwa kuwa nimeshaona jinsi ambavyo tumekuwa na maelewano mazuri uwanjani.

“Lakini pia ili nitimize malengo hayo nataka kuendelea kupigania nafasi ndani ya Simba ambayo nayo ina makipa wenzangu bora wakiwemo mzoefu Aishi Manula, Hussein Abel na Ally Salim, wote hawa nawaheshimu kwa kuwa wameshafanya mambo makubwa sana wakiwa na Simba,” alisema Camara ambaye kwenye michezo mitatu ya mashindano aliyocheza amesharuhusu bao moja alilofungwa na Maxi Nzengeli kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Lay Matampi ambaye msimu uliopita alikuwa Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara, ana rekodi ya kucheza mechi 24 kati ya 30, ikiwa ni msimu wake wa kwanza katika ligi.

Akiwa amecheza mechi 15 bila ya kuruhusu bao ‘Clean Sheet’ 15, aliisaidia Coastal Union kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho msimu huu wakimaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, hata hivyo kipa huyo raia wa DR Congo hajadaka kwenye mchezo wowote wa mashindano akiwa na Coastal Union msimu huu wakati timu hiyo ikishuka dimbani mara tatu.

Kwa upande wa Djigui Diarra amecheza misimu mitatu huku miwili akiwa Kipa Bora wa Ligi Kuu, ana rekodi ya kuifikisha Yanga Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023 na 23/24 kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu uliopita alimaliza akiwa amecheza michezo 14 ya Ligi Kuu Bara bila kuruhusu bao katika mechi 21 kati ya 30.

Aishi Manula ambaye ni kipa mzawa amekuwa bora kwa muda mrefu kwenye ligi, msimu uliopita hakupata nafasi sana ya kucheza baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na mchezo wenye kumbukumbu kubwa kwake ni kichapo cha mabao 5-1 kwenye mchezo wa Dabi dhidi ya Yanga.

Kwa upande wa Ally Salim ambaye alikuwa mbadala wa Manula, naye hakucheza mechi nyingi kwa kuwa langoni alikaa Ayoub ambaye alionyesha ubora wa juu.

Simba wameanza mambo yao mapema kuwafuatilia wapinzani wao katia hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo kwa asilimia kubwa wanakwenda kucheza dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ambao tayari mchezo wa kwanza wameifunga Uhamiaji mabao 2-0.

Katika kuhakikisha Simba inafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, imepanga kumtuma mtu wao maalum wa kwenda Libya kuwasoma vilivyo Al Ahli Tripoli katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Uhamiaji utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Tripoli nchini humo.

“Mipango ya kufanya vizuri michuano ya kimataifa inaendelea na wiki hii kuna mtu wetu ataenda Libya kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa marudiano kati ya Al Ahli Tripoli dhidi ya Uhamiaji.

“Tunataka kuwafahamu vizuri wapinzani wetu namna mbinu zao zilivyo ili kupata mwanga wa nini tunapaswa kwenda kukifanya tukielekea kucheza nao,” kilisema chanzo.

Simba itacheza dhidi ya mshindi kati ya Al Ahli Tripoli na Uhamiaji katika hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kufuzu makundi ambapo timu hiyo malengo yao msimu huu ni kuona wanafika hadi fainali.

Related Posts