Dodoma. Jeshi la Polisi Nchini litaanza msako wa vyombo vya moto ambavyo vitakuwa havijakaguliwa hadi kufikia Septemba Mosi,2024.
Mbali na hilo, jeshi hilo limesema ajali za usiku baada ya mabasi ya abiria kuruhusiwa kusafiri usiku na zinazotokana na madereva wa Serikali zimepungua.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Agosti 21,2024 na Kamanda wa Usalama wa Barabarani, Ramadhan Ng’azi alipokuwa akielezea kuhusu wiki ya usalama wa barabarani itakayoanza Agosti 26 hadi 30, 2024.
Amesema magari yasiyokaguliwa hayaruhusiwi kuwa barabarani kwa sababu ndio njia pekee ya kupambana na changamoto ya ajali nchini zinazosababishwa na ubovu wa magari.
“Kama wapo wanaokwepa (kukaguliwa), tutawafikia walipo kwa sababu wao ni kioo na sisi ni jiwe hatuwezi kushindwa na watu wowote hasa wavunjifu wa sheria. Sisi tunawataka wamiliki wa vyombo vya moto kwenda kukagua kwa hiari,”amesema.
Amesema baada ya kumalizika kwa wiki ya usalama wa barabarani wataanza msako kwa wale ambao watakuwa hawajakaguliwa na kupatiwa stika za usalama.
Aidha, Kamanda Ng’azi amesema shughuli mbalimbali zitafanyika katika wiki ya usalama wa barabarani ikiwa ni pamoja na maonyesho ya bidhaa na huduma yatakayofanyika katika uwanja wa Jamuhuri.
Amesema mgeni rasmi katika wiki hiyo itakayoambatana na jublee ya miaka 50 ya Baraza la Usalama wa Barabarani ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.
Kuhusu safari za usiku, Kamanda Ng’azi amesema mkakati walioufanya baada ya kurejeshwa kwa safari za usiku ni pamoja na kila basi linalosafiri zaidi ya saa nane kuwa na madereva wawili.
Mikakati mingine ni kila basi la abiria kuwekewa vidhibiti mwendo, kuongeza idadi ya magari ya doria na kuwapima ulevi madereva.
Amesema tangu utaratibu wa safari za usiku uanze, hakuna ajali za kutisha zilizowahi kujitokeza na kuwa zinazotokea ni ndogo.
Amesema pia walifanya ukaguzi wa leseni za udereva wale ambao hawakuwa na sifa waliwaondoa katika madaraja waliyokuwa ya leseni.
“Kwa hiyo yote haya ukiyajumuisha tumeweza kudhibiti (ajali). Lakini bila kusahau mkono wa Mwenyezi Mungu kwa sababu waumini mbalimbali wanaomba na sisi tunaomba,”amesema.
Kwa upande wa madereva wa Serikali wanaolalamikiwa kuendesha kwa fujo, Kamanda amesema takwimu walizonazo zinaonyesha vitendo vya uendeleshaji ovyo kwa madereva wa Serikali vimepungua.
Amesema takwimu zinaonyesha hadi kufikia Agosti mwaka huu, ajali zinazohusisha madereva wa Serikali na taasisi za umma zilikuwa ni 32 tofauti na mwaka jana ambapo hadi Desemba ajali 200 ziliripotiwa.
Amesema kupungua kwa ajali hizo kumechangiwa na kuwaondoa madereva wasio na sifa, kuongezeka kwa vyuo vya udereva pamoja na utoaji wa semina.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Barabarani Mkoani Dodoma, Faustine Mwakalinga amesema wamesema maonyesho hayo ni muhimu kwa wadau wa usalama wa barabarani.