Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali imejipanga kutumia mkutano wa wadau wa kimataifa wa sekta ya madini, kutangaza utajiri wa madini yaliyopo ili kuwavutia wawekezaji.
Mkutano huo ulioandaliwa na Chemba ya Migodi Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Madini unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21 mwaka huu ukiwa na kauli mbiu ya ‘uongezaji thamani madini kwa lengo la kukuza na kuendeleza maendeleo ya jamii kiuchumi’.
Mkutano huo utawakutanisha wadau 1,500 wa ndani na wa kimataifa ikiwemo Australia, Marekani, Russia, Afrika Kusini na Ghana ambapo watabadilishana mawazo na kushauriana namna bora ya kuendeleza sekta ya madini kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa.
Akizungumza Dar es Salaam leo Agosti 21,2024 katika hafla ya maandalizi ya mkutano huo, Waziri Mavunde amesema mkutano huo utakusanya wataalamu, wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa. “Hivyo hiyo ni sababu ya Serikali kujipanga kuhakikisha wanayajua vema madini yanayopatikana nchini na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo,”
“Tanzania tuna madini mengi hasa yale ya kimkakati, kama nickel, aluminium, manganese, cobalt, lithium na kinywe (graphite) yanayotumika kutengenezea bidhaa kama betri zinazotumika kwenye tochi, tutawakaribisha waje kuwekeza,” amesema
Amesema katika uwekezaji huo Serikali haitakubali kutoa leseni kwa wawekezaji kufanya shughuli hizo nchini kama hawatakuwa tayari kuridhia kuyaongeza thamani hapahapa nchini.
“Ni dhamira ya Serikali lazima tuongeze thamani madini yetu ndani ili tuweze kunufaika na raslimali hii, na mageuzi haya yalianza tangu mwaka 2017 kwa kuanza kufanya mabadiliko ya sheria inayotaka utekelezwaji wa uongezwaji thamani ya madini hapa nchini,” amesema Mavunde
Mavunde amebainisha kuwa Serikali ikiacha kusafirisha madini ghafi nje ya nchini na kujikita kwenye uongezaji thamani katika rasilimali hiyo pato la nchi na nafasi za ajira kwa vijana vitaongezeka.
“Serikali imedhamiria, hivyo tunategemea kupitia mkutano huu utakuwa wenye manufaa na tija, pia utasaidia kukuza na kuchochea ukuaji wa shughuli za sekta ya madini nchini,” amesema
Amesema ni fursa kwa Watanzania kujitokeza katika mkutano huo kwa kuwa utakusanya wataalamu na wafanyabiashara wa sekta hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Katibu wa Migodi Tanzania, Benjamin Mchwampaka amesema wanachama wao wengi watahudhuria mkutano huo na wawekezaji wa nje waliowekeza nchini, huku akieleza itakuwa siku ya Tanzania kunadi utajiri wake wa madini.
“Teknolojia mbalimbali za uchimbaji wa madini na uchenjuaji zitaonyeshwa, mijadala mbalimbali itafanyika ya kuonyesha mambo yanayofanyika kote duniani na ni fursa kwa Watanzania kujifunza kwa waliopiga hatua wanafanya nini,” amesema.
Amesema sheria za nchi zinaruhusu uwekezaji kwa mzawa na mgeni kwa mwenye mtaji unaohitajika.