Tido Mhando afichua kilichoiponza Tanzania Olimpiki – 3

Nami pia nikapata bahati ya kwenda kote, Algiers na Edmonton.

Kama kawaida kote umaarufu uliojengeka wa wanamichezo wa Tanzania ulionekana bayana waliogopewa na kuheshimiwa. Jambo moja walilokuwa nalo wanamichezo wengi wa Tanzania siku zile ni ari na jeuri kubwa ya kupambana uwanjani ikiongezewa na kujiamini. Hii ilitokana na maandalizi ya uhakika waliyokuwa wakipatiwa.

Kwa mfano kwenye michezo ya Edmonton, Filbert Bayi kwenye mbio za mita 1500 kwa mshangao wa wengi alishindwa na mkimbiaji wa Uingereza David Morecraft ambaye alikuwa hajulikani kabisa.

Lakini wakati tunajiuliza kumetokea nini, ghafla kambi ya Tanzania ikapata mshangao wa ushindi mkubwa ambao haukutarajiwa.

Kufuatana na taratibu za mchezo wa mbio za marathoni, mkimbiaji hushauriwa kutoshiriki kwenye mbio nyingine za masafa hayo hadi baada ya kupita miezi 3 tangu akimbie kwenye mbio nyingine hizo.

Sasa kama nilivyosema timu ya Tanzania iliyoshiriki kwenye michezo ya Afrika ndiyo hiyo hiyo iliyokwenda kwenye michezo ya Jumuiya za madola. Kwa bahati mbaya wakimbiaji wetu wa marathon hawakuweza kufanya vizuri Algiers na kulingana na taratibu nilizozieleza awali, hatukuwa na timu ya kukimbia marathon huko Edmnton.

Kwa ujumla baada ya kushindwa kwa Filbert Bayi, ingawaje alipata medali ya fedha lakini kambi ya Tanzania ilikosa raha kabisa.

Sasa kwenye michezo hiyo ya Canada mbio za marathon zlipangwa kuwa za mwisho kabisa. Kwa mshangao wa wengi mmoja wa wakimbiaji wetu wa marathon aliyeshiriki Algiers, Gidamis Shahanga akashikilia kutaka tu ashiriki kinyume cha taratibu zilizopo.

 Baada ya mazungumzo marefu hatimaye akakubaliwa ingawaje wengi wetu tulidhani anakwenda kujifurahisha tu. Mimi binafsi niliamua kuzipuuza mbio hizo na kurejea hotelini kwangu ili kuandaa ripoti yangu mapema. Kwa bahati chumbani kulikuwa televisheni ingawa miaka hiyo Tanzania kulikuwa hakuna.

Ghafla nikamsikia mtangazaji anataja jina la Shahanga kwa msisimko mkubwa kwamba alikuwa tayari anampita mkimbiaji aliyekuwa mbele wa kwanza tena akiwa bado na nguvu sana na kuwa umbali uliobakia ulikuwa mdogo sana.

Nilishikwa na butwaa,hotelini nilikokuwa ilikuwa ni mbali sana na kiwanjani. Sikuwa na ujanja bali kurekodi sauti ya mtangazaji yule wa televisheni wa lugha ya Kiingereza hadi Shahanga anamaliza wa kwanza na kutushangaza wengi.

Lakini hiyo ndiyo iliyokuwa sifa kubwa ya wanamichezo wa Tanzania wa michezo yote miaka hiyo ya 70 na 80, kupambana hadi tone la mwisho.

Labda katika kudhihirisha hilo niwapatie mfano mwingine, ulio maarufu sana kwa wengi wana mchezo nchini, kwakuwa unaihusu klabu kubwa ila ntaieleza hadithi hiyo kwa jinsi nilivyoishuhudia mimi.

Ilikuwa mwaka 1979,nami nilikuwa mtangazaji wa pambano la klabu bingwa ya kandanda Afrika, mkondo wa kwanza, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baina ya Simba na Mufulira Wanderers ya Zambia.

Matokeo ni Simba kuathibiwa kipigo cha bao 4-0 mbele ya mashabiki wao. Aibu iliyoje. Hakuna aliyetaka kujua kuhusu mechi ya marudiano mjini Lusaka wiki mbili baadaye. Ikaelezwa kwamba hata uongozi wa klabu ya Simba wenyewe wasiipeleke timu bali walihofia kubanwa na sheria ngumu za mashindano hayo.

Wakaamua kuipeleka timu kwa treni ya Tazara. Watu pekee waliokuwa na matumaini angalau ya ushindi mdogo walikuwa ni wachezaji na mwalimu wao Joel Bendera. Ilikuwa kikosi cha vijana wa Kitanzania pekee  hakukuwa na raia yoyote wa kigeni. Kwakuwa nilikuwa mtangazaji wa kipindi  cha michezo nilikuwa miongoni wa watu wachache sana tuliokwenda kwenye stesheni ya Tazara kuiona timu hiyo ya Simba ikiondoka.

Hakuna mwandishi wa habari hata mmoja aliyekuwemo kwenye msafara huo na wala Radio Tanzania haikufanya utaratibu wa kuitangaza mechi hiyo mubashara.

Kama kawaida kufuatia mzaha wa watani wa jadi, pale Radio Tanzania pia watu walikuwa wakitaniana sana. Sasa siku yenyewe ya mchezo ambayo ilikuwa ni siku ya Jumamosi, mkurungenzi wa Habari wakati huo Sam Mdee akiwa amehamishiwa kutoka Ikulu, katika hali ya kutaka kuwachochea watani wake, yeye alikuwa Yanga damu, akaniita, akaniambia, kwakuwa mchezo wenyewe tulikuwa hatuutangazi laivu, basi niufuatilie tu kwa njia zangu na kila linapotokea jambo muhimu na hasa magoli, nikatishe matangazo ya kipindi cha kawaida na kutangaza goli hilo.

 Nilitegemea kupata taarifa za mechi hiyo kutoka kwa chumba cha habari cha Radio Zambia Lusaka. Nilichelewa kupata laini ya simu, lakini nilipopata kama dakika 20 baada ya mchezo kuanza, mwandishi wa Radio Zambia akanifahamisha kuwa Simba walikuwa tayari wanaongoza kwa mabao 2-0. Nikawaambia wasinitanie, akanihakikishia ni kweli, nikaenda kutangaza. Watanzania wengi hawakuamini. Hata Mdee nàe alinipigia, nikamwambia ni kweli. Nikapiga tena simu muda mchache baada ya filimbi ya mapumziko, jamaa zangu wakaniambia ni mapumziko lakini Simba walikuwa wanaongoza kwa magoli 3, hata mimi sikuamini, nikaenda kutangaza, jiji la Dar likanza kutetema.

Nilisubiri kama robo saa hivi baada ya kipindi cha pili kuanza kwa mshangao mwingine mkubwa nikaambiwa Simba walikuwa wamefunga bao la 4, maajabu yametokea. Nikaenda kutangaza. Simu nyingi zikaanza kupigwa, hakuna aliyeamini, Simba kupata magoli yote hayo dhidi ya Mufulira, uwanjani mjini Lusaka tena mbele ya kiongozi wao, Rais Kenneth Kaunda, timu iliyowatia aibu Dar? loooh maajabu makubwa.

Nilisubiri kwa muda hadi kama bado dakika 10 hivi mchezo kumalizika, nikauliza tena, safari hii  nikaambiwa tayari Simba walikuwa wamefunga bao la 5, yaani Simba 5 Mufulira Wanderers 0.  Historia imeandikwa. Mayoe na vifijo vikasikika.Simba inasonga mbele kwenye michuano hiyo ya Afrika. Hakuna aliyeamini hadi kikosi kile cha vijana wa Kitanzania watupu kiliporejea nchini na kuelezea hadithi yote. Maelfu ya mashabiki safari hii walifurika Tazara kuwapokea mashujaa hao. Huu ni mwaka wa 45 sasa tangu rekodi hii kuwekwa na bado haijavunjwa na klabu nyingine yoyote Afrika.

Nimejaribu kwa kadri nilivyoweza kwenye makala hizi kuelezea mafanikio makubwa yaliyoletwa na wanamichezo wetu na kuipatia sifa kubwa Tanzania kwenye miaka hiyo ya 70 na 80 kwa kushinda kwenye michezo mikubwa ya kimataifa tena kwa ujasiri mkubwa.

Hali iliyo tofauti sana na sasa. Iweje siku hizi tuonekane dhaifu kwenye michezo mingi na hata kushindwa na majirani zetu ambapo hapo awali tulikuwa tukiwatambia?

Tunawajibika kufanya tafakari ya kina na wala si ya kubabaisha. Je,tupo sahihi kukumbatia sana mchezo mmoja na kuitelekeza mingine? Na hata kwenye huo mchezo mmoja yaani kandanda, mbona tunaonekana kuwashabikia zaidi wachezaji wa kigeni? Je, tuko sahihi kwa kufanya hivyo wakati huu michezo inachukua sehemu stahiki ya ajira kwa vijana katika mataifa mengi duniani?

Hapana shaka kwa ushahidi huu wa mafanikio yetu michezoni kwenye miaka hiyo ya nyuma vijana wa  Kitanzania wana vipaji vikubwa tu vya kuweza kutamba tena kwa jeuri kubwa miongoni mwa vijana wengine duniani kwenye michezo mbalimbali. Kinachotakiwa ni kuwepo kwa mipango, mikakati na dhamira ya kweli ya kutaka mafanikio ya uhakika, vinginevyo kama ilivyokuwa kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu huko Paris, Ufaransa, tutaendelea kuvuna tunachopanda.

Related Posts