MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), inatarajia kuendesha mafunzo ya rada kwa nchi za Afrika Mashariki pamoja na zile za Ukanda wa Kusini mwa Afrika ambayo yataanza kufanyika tarehe 26 Agosti, mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Fursa hiyo imeipata TMA kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa zikiwemo rada uliofanywa na Serikali ya Tanzania katika utabiri wa hali ya hewa pamoja na matokeo chanya katika sekta hiyo.
Akifungua Semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya masuala ya utabiri wa hali ya hewa leo tarehe 21 Agosti 2024 jijini Dar es Salaam, Dk. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (TMA), amesema kuwa fursa hiyo imeipata Tanzania baada Shirika la Hali ya hewa Duniani (WMO), kujiridhisha kuwa Tanzania inaweza kuendesha mafunzo hayo kutokana na uwekezaji wa miondombinu ya hali ya hewa.
Dk. Chang’a ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa duniani (WMO) amesema mafunzo hayo yataendeshwa jijini Mwanza tarehe 26 Agosti kwa watendaji wa Mamlaka Hali ya Hewa katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
“Ndani ya miaka mitatu kumekuwa na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya utabiri wa hali ya hewa zimetuwezesha sisi wataalamu kupata umahiri na uweledi,” amesema Dk. Chang’a ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC ).
Amesema kuwa uwekezaji huo umeifanya Tanzania kukosa ushindani na kupelekea kupewa nafasi hiyo ya kuzifundisha matumizi ya teknolojia ya rada nchi hizo.