Songwe. Majengo ya Shule ya Msingi Iyuli iliyopo kata ya Mlale wilayani ileje mkoani Songwe yapo hatarini kubomoka kutokana na kuta za majengo hayo kuzungukwa na nyufa, huku wanafunzi wakihofia usalama wao.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1993 ambapo wananchi na Serikali walisaidiana kujenga, kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wanasafiri umbali wa kilomita 12 kutoka kijijini hapo, kufuata masomo katika Shule ya Msingi Itumba iliyoanzishwa mwaka 1961 iliyopo yalipo makao makuu ya wilaya ya Ileje.
Kutokana na ubovu wa majengo ya shule hiyo, wanafunzi wanalazimika kuziba baadhi ya nyufa kwa tofali lengo likiwa ni kujilinda na upepo mkali wakiwa darasani, hali ambayo imeelezwa kufifisha jitihada za wanafunzi kuhudhuria masomo shuleni hapo.
Luka Mnkondya mkazi wa kijiji hicho amesema, “kutokana na uchakavu wa majengo ya shule yetu, kipindi cha masika Mungu anasaidia wanafunzi kumaliza siku salama, kwani muda wowote kuta za vyumba vya madarasa zinaweza kuanguka kama unavyoona mwandishi, hata sisi wazazi hatuna amani na wanafunzi wanaposomea kwenye vyumba hivi.”
Jailosi Mtindya amesema kwa sasa shule hiyo imebaki kama magofu, huku viongozi wakiahidi kutenga bajeti kila mwaka wa fedha ya kujenga vyumba vipya vya madarasa, bila mafanikio.
“Shule hii imebaki kama sehemu ya kuishi mifugo kitendo ambacho ni kuhatarisha maisha ya wanafunzi na walimu wanapotekeleza majukumu yao, hivyo tuiombe Serikali isikilize kilio cha wananchi kuondoa changamoto hii ya uchakavu wa majengo ya shule,” amesema Mtindya.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Neema Anyelwisye amesema majengo ya shule hiyo hayapo katika hali nzuri, kwani wanafunzi wanaingiwa hofu ya kuangukiwa na kuta pindi wawapo darasani.
“Tunaomba Serikali itusaidie kutatua changamoto hii kwani baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuhudhuria masomo wakihofia usalama wao.”
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 212 wakiwamo wa kiume 124, huku walimu wakiwa tano wakiwamo wa kike watatu, ambapo vyumba vya madarasa vinavyotumika na vina hali mbaya ni vitano huku mahitaji yakiwa vyumba vinane.
Diwani wa kata ya Mlale, Yotham Ndile amesema wanafunzi wa shule hiyo wapo katika hatari ya kuangukiwa na kuta kutokana na uchakavu wa majengo, lakini bado Serikali haijatenga hata bajeti ya ujenzi wa vyumba vingine.
Naye, Kaimu Ofisa Elimu Msingi wilayani humo, Bonventure Kilongozi amesema shule nyingi za msingi wilayani humo zinakabiliwa na uchakavu wa majengo ikiwamo Iyuli.
Amesema wanatarajia kutenga fedha kidogokidogo kuboresha miundombinu hiyo.