MAMBO ni mazuri kwa timu za Upanga, Pak Stars na Caravans baada ya kuibuka wababe mechi za kriketi kuwania Kombe la TCA jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Zilikuwa ni mechi za mizunguko 50 ambazo zilichezwa kwenye viwanja vya Dar Gymkhana na Leaders Club na hivyo kuwapa burudani wapenzi wa mchezo wa kriketi.
Mechi kati ya Aga Khan Sports na Upanga ndiyo ilikuwa gumzo la jiji mwishoni mwa juma kutokana na kuwepo kwa wachezaji wenye majina makubwa katika mchezo huu.
Timu hizi zilichezwa kwa ustadi mkubwa lakini ni Upanga ndio walioibuka vinara kwa ushindi mwembamba wa wiketi 2 hadi mwisho wa mchezo.
Aga Khan ndio walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 231 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko yote 50.
Kwa jitihada kubwa, vijana wa Upanga waliivuka idadi ya mikimbio ya wapinzani wao kwa kupiga mikimbio 232 na kupoteza wiketi 8 huku wakitumia mizunguko 48 kati ya 50 iliyowekwa.
Mchezaji Abhik Patwa wa Aga Khan aling’ara kwa kutengeneza mikimbio 94 peke yake, lakini haikuisaidia timu yake kuepuka kichapo.
Kwa upande wa washindi alikuwa ni Ramesh Alluri aliyeangusha wiketi 3 za wapinzani akisaidiwa na Asuri Rajendra aliyeangusha wiketi 2 na Rishen Patel aliyepata wiketi 2 ndiyo walioisadia sana timu yao kushinda mchezo huo.
Pia, waliong’ara sana mwishoni mwa juma ni vijana wa timu ya Pak Stars ambao waliifunga Aces A kwa wiketi sita katika mchezo mkali uliochezwa pia mwishoni mwa juma.
Aces A ndiyo walioshinda kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 140 baada ya wapigaji wao wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 37 kati ya 50.
Kwa utulivu mkubwa, vijana wa Pak Stars A waliweza kuzifikia na kuzivuka alama za wapinzani wao kwa kutengeneza mikimbio 146 huku wakiangusha wiketi 4 na wakitumia mizunguko 27 kati ya 50 iliyowekwa.
Zafar Khan aliyeangusha wiketi 4 za wapinzani na Mohamed Ali aliyepata wiketi 3, ndiyo walioisadia timu ya Pak Stars kupata ushindi wa wiketi 6 katika mchezo huo.
Lakini mambo hayakuwa mazuri kwa timu B ya Pak Stars ambayo ilichezea kichapo cha wiketi 10 kutoka kwa timu ya Caravans.
Pak Stars B ndio walioanza kubeti lakini wote wakatolewa wakiwa wametengeneza mikimbio 83 na hivyo kuwapa kazi rahisi vijana wa Caravans waliotengeneza mikimbio 84 bila ya kupoteza wiketi. Walitumia mizunguko 11 tu kati ya 50 iliyowekwa.
Akhil Anil aliyeangusha wiketi 3 za wapinzani alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliong’ara katika mechi hiyo.