‘Viongozi wa dini epukeni kauli za uchochezi’

Dar es Salaam. Viongozi wa dini wameaswa kujiepusha na kauli za uchochezi na uvunjifu wa amani unaoweza kusababisha nchi kuingia katika machafuko, badala yake kuhubiri amani na upendo.

Hayo yameelezwa leo Agosti 21, 2024 na Mratibu Mkuu wa Taasisi ya Sambaza Upendo, Amani na Umoja, Banzai Suleiman baada ya kutoa misaada kwa wajane na watu wanaoishi katika mazingira magumu katika makao makuu ya Msikiti wa Shia Ith Tanzania na Sheria Kigogo (TIC) Dar es Salaam.

Suleiman ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la Kamel, amesema viongozi hao wanatakiwa kutumia vipawa vya kiroho katika kuendeleza masuala ya upando na amani katika nchi yetu.

“Wapo viongozi wa dini wanaokwenda kinyume ili Watanzania wakose upendo, amani na umoja tutahakikisha tunawataja moja kwa moja kwa sababu kama Mungu ametufikishia tunu hii. Wewe ni nani unayetutenganisha?” amehoji Suleiman.

Amesema lengo la taasisi hiyo ni kuona Watanzania wakiwemo vijana wa dini zote wanaopata mafunzo ya kiufundi ili yaweze kuwasaidia kuondoa changamoto mbalimbali za kimaisha.

Mjumbe wa bodi wadhamini ya Jumuiya ya TIC, Sheikh Mohamed Abdi amesema kila kiumbe kinapaswa kuishi kwa amani na upendo.

“Mtume wetu Muhammad (S.A.W) hajasifiwa kwa kusali bali alisifiwa kwa kuwasaidia watu waliomzunguka na wenye itikadi mbalimbali,” amesema Sheikh Abdi.

Pia ameishukuru taasisi hiyo kwa kuisaidia jamii wakiwemo makundi ya wahitaji kama ambavyo tunavyoelekezwa katika vitabu vya dini.

Naye Askofu wa Kanisa la Golani Christian, Dk Leonard Ntibanyiha amesema kutoa misaada kwa wajane na wazee ndio lengo la taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2018.

Related Posts