Wacheza gofu watano viwanjani Entebbe Uganda Open

BAADA ya Madina Idd kushinda mashindano ya wazi wa gofu ya wanawake nchini Uganda, wacheza gofu watano kutoka Tanzania wako viwanjani kusaka ubingwa wa mashindano ya wazi ya Uganda yanayoanza asubuhi hii kwenye viwanja vya gofu vya Entebbe nchini humo.

Ni mashindano makubwa ambayo mdhamini wake mkuu kampuni ya John Walker amemwaga mzigo wa Sh500 milioni za Uganda (sawa na Sh360 milioni za Tanzania) kama zawadi.

Timu ya Watanzania watano inaongozwa na katibu wa chama cha gofu ya wanawake (TLGU), Yasmin Challi na imeshawasili Entebbe.

Wawakilishi wengine wa Tanzania ni ‘Malkia wa Swing’ Vicky Elias na Hawa Wanyeche kutoka klabu ya Lugalo ya Dar es Salaam wakati Neema Olomi (Arusha Gymkhana) na Loveness Mungure (Kili Golf Club) wanatokea Arusha.

“Tupo vizuri na tumejiandaa vyema kwa mashindano haya. Naamini tutafanya vizuri kama tulivyofanya katika mashindano ya wazi ya Pwani ya Kenya,” alisema Vicky.  

Kabla ya kwenda Uganda  Neema, Vicky na Yasmin Challi walifanya vizuri katika mashindano ya wazi ya Kenya yaitwayo Coastal Ladies Open na kuiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili nyuma ya wenyeji.

Olomi alimaliza katika nafasi ya pili wakati Vicky alishika nafasi ya tatu katika mashindano yaliyojumuisha viwanja vitano tofauti katika miji ya Mombasa, Malindi na Vipingo.

Yasmin alishinda kwa upande wa wastani wa fimbo kwa kupiga mikwaju 72.

Related Posts