Wagonjwa 12 hufanyiwa upasuaji wa ubongo, mgongo Bugando

Mwanza. Watu saba wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo na tatizo la mgongo, miongoni mwa 12 wanaotakiwa kupatiwa tiba hiyo kwenye kambi maalumu ya siku tano iliyoanza Agosti 19, 2024 na inatarajiwa kukamilika Agosti 23, 2024 katika Hospitali ya Bugando.

Jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza na Chuo Kikuu cha Tiba cha Vanderbilt cha nchini Marekani, wamefanikisha upasuaji huo.

Wagonjwa wenye hali mbaya wanaohudhuria matibabu katika idara ya upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu wakipewa kipaumbele katika matibabu hayo.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 21, 2024, ndani ya chumba cha upasuaji, Daktari Bingwa wa ubongo na uti wa mgongo, kwenye Hospitali ya  Bugando, Gerald Mayaya amesema wagonjwa watano kati ya 12 waliofanyiwa upasuaji huo wana uvimbe kwenye ubongo, huku saba wakisumbuliwa na tatizo la mgongo.

Dk Mayaya amesema (bila kutaja idadi) tatizo la watu kukutwa na uvimbe kwenye ubongo na maumivu ya mgongo ni mwiba kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, huku akitaja baadhi ya visababishi kuwa ni pamoja na ajali, matatizo ya kuzaliwa nayo na watoto kuzaliwa na tatizo la vichwa kujaa maji kupitiliza.

“Kwa wenye uvimbe kwenye ubongo tunauondoa na wenye matatizo kwenye uti wa mgongo na wanahitaji kupandikiziwa pingili za bandia tunafanya hivyo. Tumeungana na wenzetu kutoka Hospitali ya Vanderbilt ya nchini Marekani ambao wametupatia ujuzi mpya wa kufanya upasuaji huu,” amesema Dk Mayaya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bugando, Dk Fabian Massaga, Mkurugenzi wa Huduma za Afya Saidizi, Dk Cosmas Mbulwa amesema kati ya wagonjwa 11,000 wanaohudhuria kliniki ya upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, 1,200 sawa na asilimia 11 hufanyiwa upasuaji huo.

Dk Mbulwa amesema takwimu zinaonyesha wastani wa wagonjwa 5,940 sawa na asilimia 54 ya wote (11,000) wanaotibiwa katika kliniki ya upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ni wanawake huku wagonjwa 5,060 sawa na asilimia 46 wakiwa wanaume.

Amesema kati yao, wastani wa wagonjwa 1,375 sawa na asilimia 12.5 wanakutwa na tatizo la uvimbe kwenye ubongo, wagonjwa 880 sawa na asilimia nane wana shida za mgongo, wagonjwa 3,300 sawa na asilimia 30 ni watoto wenye tatizo la vichwa kujaa maji kupita kiasi, huku asilimia 49.5 wakisumbuliwa na matatizo mengine ikiwemo changamoto za ajali.

“Kambi hii imelenga zaidi kwenye upasuaji mkubwa wa ubongo na mgongo, matarajio yetu ni kuwafanyia upasuaji wagonjwa 12 na kuona wagonjwa wa nje zaidi ya 100,” amesema Dk Mbulwa.

Amewataja madaktari bingwa kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Vanderbilt  kuwa ni Dk Christopher Bonfield, Dk Reid Thompson, Dk Soren Jonzzon na Muuguzi mbobevu, Elizabeth Haley Vance.

Mkazi wa Meatu mkoani Simiyu, Wande Paulo (19) akizungumza huku akiwa amelala kitandani siku moja baada ya kuondolewa uvimbe kichwani amesema hali ilikuwa tete, lakini baada ya upasuaji huo afya yake imeanza kuimarika huku akilishukuru jopo la madaktari hao kwa kunusuru uhai wake.

“Mwanzoni nilikuwa nasikia maumivu makali kichwani na kizunguzungu cha kila mara kiasi kwamba sikuweza kufanya shughuli yoyote, baada ya kupimwa nilikutwa na uvimbe kwenye ubongo ndipo nilipofika Bugando. Nawashukuru wamenifanyia upasuaji naendelea vizuri,” amesema Wande.

Mama mzazi wa Wande, Mariam Charles amesema kutokana uvimbe uliokuwa ukimsumbua binti yake alisitisha shughuli za uzalishaji ili kumhudumia ikiwemo kumpeleka kwa waganga kienyeji, ambako hakupata msaada wowote hadi alipomfikisha Bugando na kufanyiwa upasuaji huo.

“Kwa kweli anaendelea vizuri mno, alikuwa hawezi hata kufanya shughuli yoyote lakini baada ya kufanyiwa upasuaji ndani ya siku moja fahamu zake zimerudi na anaendelea vizuri. Nawashukuru sana hawa madaktari na Hospitali ya Bugando, Mungu awabariki,” amesema.

Kambi hiyo ni moja ya jitihada za Hospitali ya Bugando kukita mizizi kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na kibingwa bobezi, sambamba na kuifanya hospitali hiyo kuwa Kituo Kikuu cha Utalii wa Matibabu (Medical Tourism) nchini na Afrika Mashariki.

Related Posts