Walima tumbaku Tabora walalama kunyimwa mikopo na taasisi za fedha

Tabora. Baadhi ya wakulima wa tumbaku mkoani hapa waliopata hasara katika msimu wa kilimo wa 2023/24, wamezilalamikia benki kuwanyima mikopo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo.

Inaelezwa kuwa hasara hiyo ilisababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwaka jana na mwanzoni mwaka huu ambazo ziliharibu  tumbaku yao shambani na kuwafanya wengi wao kushindwa kulipa madeni ya awali.

Akizungumza na Mwananchileo Jumatano Agosti 21, 2024, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Useguzi, Ally Mrisho amesema wanachama wake wengi wamekosa mikopo kwa sababu bado wanadaiwa kutokana na hasara waliyoipata.

Zao la Tumbaku ambalo ni maarufu Tabora likiwa limenawiri shambani. Picha na Johnson James

Amesema hasara ya msimu uliopita ilifikia Dola 75,000 za Marekani (zaidi ya Sh190 milioni) na mikopo ingewasaidia wakulima kuendelea na shughuli zao za kilimo.

Naye Robert John, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Ugaga mkoani humo, amesema hasara iliyopatikana kwa msimu wa 2023/2024 haijawahi kutokea.

 “Mwaka jana tulipata hasara kubwa kutokana na mvua nyingi ambazo zilisababisha maji kusomba mbolea kutoka kwenye mizizi ya tumbaku, na hivyo kuharibu mazao. Tunaiomba Serikali itusaidie katika mikopo,” amesema John.

Akilizungumzia hilo, Meneja wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi, Abert Charles amesema mvua hizo zimesababisha hasara pia hata kwa bodi yao.

“Kwa msimu uliopita tulitarajia kuzalisha zaidi ya kilo 104 za tumbaku, lakini kutokana na mvua zilizoleta mafuriko, tulifanikiwa kuzalisha tani milioni 61 pekee. Hii ni hasara kubwa kwa kilimo hiki,” amesema Charles.

Amesema wakulima wengi hawatakuwa na uwezo wa kuendelea kulima tumbaku kwa sababu mabani yao ya kukaushia yaliangushwa na mvua na itawachukua miaka miwili hadi mitatu kujenga upya miundombinu hiyo. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa wakulima kujiunga na bima za kilimo ili kulindwa dhidi ya hasara.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amewataka viongozi wa benki na wakulima kukaa pamoja kutafuta njia za kuwasaidia kuanza upya kilimo hicho.

“Takwimu zinaonyesha tumepata hasara kubwa, na hakuna tumbaku iliyouzwa msimu uliopita. Ninawaomba wakulima kujiunga pia na bima za kilimo ili kuepuka hasara zinazotokana na majanga yasiyotabirika kama haya,” amesema Chacha.

Related Posts