Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa wamependekeza ilani za vyama zitokane na Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Wameeleza hayo leo Jumatano Agosti 21, 2024 wakati wa mjadala wa kutoa maoni kuhusu uboreshaji wa mpango wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ulioratibiwa na Tume ya Taifa ya Mipango.
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo amesema kuna haja ya kuja na mbinu itakayosaidia ilani za vyama zitengenezwe kwa kuzingatia mipango iliyopo kwenye dira ya Taifa.
“Watu wanatoa maoni mazuri kujenga dira, lakini wasiwasi wangu tunajengaje wakati kila chama kinakuwa na vipaumbele vyake? Au itakuwa maneno tu, tunataka kutengeneza vitabu wakati DP ikitaka mambo yake inafanya,” amehoji.
Kwa mujibu wa Cheyo, ni vema Serikali ikaangalia upya kuona namna bora ya ilani za vyama ziendane na mipango ya dira ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ADC, Shaban Tutu amesema kwa kuwa dira ni jambo kubwa, ni vema Tume ya Mipango ikakaa na vyama vya siasa ili kuelimisha kama wanatakiwa kuachana na ilani zao za miaka mitano mitano.
“Inawezekana mkawa na dira, lakini vyama vikaja na ilani zao inayosema huduma za afya kuanzia mwaka 2025 itakuwa bure, lakini kwenye dira hilo halipo, maana yake unaweza kuleta mgongano. Dira haitafanya kazi na wanasiasa wanachukua nafasi kwa sababu wanajenga nchi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad amesema kila baada ya miaka mitano vyama vya siasa vinafanya uchaguzi kwa kuzinadi ilani zao, ili kukubalika kwa wananchi.
“Vyama vingi vinakuwa na ilani, CCM wana ilani yao, CUF, Chadema ilani yao ningeshauri tume hii isione uvivu ikusanye ilani za vyama hivi na kuzipitia kwa sababu kuna mambo mengi vyama vimeelezea mtaona lipi linakubalika na lipi halikubaliki,” amesema.
Katika hatua nyingine, Cheyo amesema angependa katika miaka 25 ijayo, Tanzania iwe na utaratibu utakaohakikisha watu wenye taaluma, ikiwemo ya kusoma utawala na sheria ndio wateuliwe kuwa wakuu wa wilaya ili kuondokana na hali ya ‘uchawa.’
“Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi nzuri, lakini tutaendelea na utawala wa wakuu wa wilaya wanaopatikana kwa njia ya uchawa? Ukiwa chawa mzuri unaumauma sana unakuwa DC, lakini leo sifa ya kushindwa uchaguzi unakuwa DC.
“Si kuchaguana kwa sababu unamjua mkubwa kwa sababu ni uchawa, ni muhimu watu wawe na sifa na waheshimu taaluma. Zamani tulikuwa tunakimbilia kazi serikalini kwa sababu ni sehemu ya kudumu, leo ukitaka kazi ambayo hauna uhakika unakimbilia serikalini, je kwa miaka 25 ijayo tutaendelea kuwa hivi?” amehoji Cheyo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema ili kujenga Taifa lenye kuona fursa nje ya nchi, ni muhimu kuchagua lugha ya kufundishia.
“Lugha tunayofundishia inasaidiaje kushindana au kuziona fursa, kushindana na kuzipata? Tufike mahali tuamue kama tunataka tuchague lugha ambayo tutaifahamu vizuri ili kwa miaka 25 ijayo tuweze kushindana, kama ni Kiswahili au Kiingereza,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu amesema kwa kuwa yote yanayoandaliwa katika mpango wa dira yanahitaji kutekelezwa, wanahitaji kuwa na uongozi mzuri.
“Utawala ni eneo la msingi, nani tunakwenda kumkabidhi dira hiyo kwa ajili ya kuisimamia na kuitekeleza, lazima tupate watu wenye wivu wa jambo hilo na wenye uelewa na kukubali kusimamia,” amesema.
Mwenyekiti Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo amesema kwa kuwa vijana ni kundi kubwa, ni muhimu kuanzishwe benki ya vijana itakayowawezesha kwenda kukopa kwa riba ndogo.
“Ukienda Njombe kwenye mashamba ya viazi kukodi ardhi ni Sh200,000 ukienda Wemba ardhi wanakodisha kwa Sh100,000 lakini kuna mashamba ya vijiji hayalimwi ni utaratibu upi umewekwa na Serikali kuwawezesha vijana kumiliki ardhi?” amehoji.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema, “tumekuja hapa kuangalia ni kitu gani kama wanasiasa tunaona kikiingizwa kwenye dira kitatuunganisha kama Watanzania, niwe muwazi siasa zilizopo sasa ni za ushindani zinazozaa fitina na kuchafuana.
“Kwa sababu kila anayekuja kuchukua madaraka anafuta vya aliyepita, anataka kuleta vyake na kitu kinaitwa maendeleo hatuwezi kufanikiwa kwa mfumo huo. Tukiwa na dira, inatoa uhuru hata kwa wananchi kuchagua hawa wameshindwa tuwape hawa,” amesema.
Jaji Mutungi amesema kukiwa na dira makini itasaidia Taifa kuondokana na siasa za chuki na kutanguliza uzalendo kama inavyosifiwa Marekani ikiwa kwenye harakati za kidunia wanatanguliza Taifa lao kwanza.
Awali, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema mwaka 2050 dunia itakuwa inaongozwa na mabadiliko ya teknolojia, hivyo lazima Tanzania ijiandae kushiriki katika suala hilo.
Alihoji Watanzania wanatayarishwa kwa namna gani kwa sababu kuna kazi zinazofanyika hivi sasa, ikifika miaka hiyo hazitakuwepo.
“Tunavyoangalia miaka 25 ijayo lazima tukumbuke katika ubongo wetu na tunawatayarisha Watanzania wa namna gani? Miaka 25 inayokuja kwa vyovyote mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira yatakwenda kwa kiwango cha juu,” amesema Mafuru.
Hata hivyo, amesema kabla ya kuipata dira watawaita kuwapa mrejesho kwa kila kilichochakatwa.
Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Kitalaamu ya Dira ya Mwaka 2050, Dk Asha-Rose Migiro amesema njia waliyotumia kukusanya maoni ni kupitia mahojiano ya ana kwa ana, kukutana na watu mmoja mmoja, makundi na utafiti kwa njia ya simu.
“Kumekuwa na utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi wa simu, sambamba na kutumia tovuti katika ukusanyaji wa maoni. Tumefanya mikutano, mazungumzo na asasi za kiraia, taasisi za umma na Watanzania wanaoishi nje ya nchi,” amesema.
Amesema kwa tathimini fupi baada ya kukusanya maoni, wananchi wengi wanahitaji kuona kunaundwa utaifa wa nchi na kulindwa na kuheshimu utu wa kila Mtanzania.
“Tumeyapokea maoni yote yaliyosemwa na wenzetu kwa unyenyekevu na yote tumeyasikia,” amesema.