Watoto kupotea kwailipua Simiyu kwa maandamano, mmoja adaiwa kuuawa

Bariadi. Matukio ya watoto kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika Mji wa Lamadi, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu yameibua vurugu baina ya wananchi na polisi, ambao walilazimika kutumia mabomu ya machozi kutuliza hali hiyo.

Mvutano huo ulidumu kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni ya leo Jumatano, Agosti 21, 2024. Katikati ya muda huo, wananchi walilazimika kufunga barabara kuu ya Mwanza-Simiyu-Mara kwa takriban saa tano wakishinikiza Serikali mkoani humo na Jeshi la Polisi kukomesha vitendo hivyo.

Kufungwa kwa barabara hiyo kulisababisha usumbufu kwa wasafiri na watumiaji wa njia hiyo, huku magari yaliyolazimisha kupita yakirushiwa mawe na wananchi hao. Baadhi ya wananchi wamejeruhiwa katika makabiliano hayo na polisi, zaidi ya 100 wamekamatwa huku kukiwa na taarifa za kifo, ingawa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faidha Salim, amekanusha kuwepo kifo, akisema wapo majeruhi pekee.

Sababu ya maandamano hayo ni taarifa za watoto kupotea, hali iliyowafanya wananchi hao kwenda Kituo cha Polisi Lamadi kutafuta majibu ya nini kinaendelea.

Shughuli za kijamii na kiuchumi eneo la Lamadi zilisimama. Mabomu yalirindima, huku mawe yakirushwa. Hata msafara wa kamati ya usalama wilaya chini ya DC Salim ulionja shubiri ya kushambuliwa na wananchi hao.

Ilipofika saa 1 kasoro, baadhi ya shughuli, ikiwemo maduka, yalianza kufunguliwa ingawa pia umeme ulikatika.

Polisi wenye silaha na askari kanzu walipita huku na huko kuhakikisha amani inarejea, huku DC Salim akiwaahidi wananchi kwamba hatua zitachukuliwa na kuwasihi kutulia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia mwananchi ni kuwa Meshack Paka (20) amefariki dunia kwa kudaiwa kupigwa risasi tumboni na kutokea upande wa pili.

Baba yake mdogo, Makelemu Paulini, alizungumza na Mwananchi na kusema Meshack alipigwa risasi hiyo akiwa katika Standi ya Lamadi akitafuta gari kwenda kijiji jirani cha Satiwa, alikoitwa na baba yake mzazi, Daudi Paka kumsaidia kazi.

“Meshack nilikuwa naishi naye hapa Lamadi, lakini jana alinipigia simu na baba yake mzazi akimtaka mwanaye leo aende Kijiji cha Satiwa kumsaidia kazi ya kuuza mahindi. Akiwa kituo cha Lamadi akitafuta gari majira ya saa tano asubuhi, alipigwa risasi na polisi maeneo ya tumboni na risasi hiyo kutokea matakoni,” amesema Makelemu.

“Kweli nilipofika, nilimkuta akigalagala, ndipo tukakodi usafiri kumpeleka hospitali ya Mukula, lakini kabla ya kufika alifariki njiani. Ikawa mwisho wa maisha yake na mwili tumeuhifadhi katika hospitali ya Nyashimo. Hivi sasa (saa 7:26 usiku) tuko Kituo cha Polisi Lamadi tunaandika maelezo pamoja na baba wa marehemu, Daudi Paka,” amesema.

Makelemu amesema Meshack alimaliza kidato cha sita mwaka huu na alipata matokeo mazuri (Daraja la Kwanza la alama sita), na walikuwa kwenye mchakato wa kumpeleka chuo.

Tukio hilo linatokea zikiwa zimepita siku 32 tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka machifu na viongozi wa mila kukemea vitendo kama hivyo katika ngazi za chini wanakotoka. Rais Samia alieleza hayo Julai 20, 2024, alipokutana na machifu wote nchini, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, akisema mauaji ya watu wenye ualbino na utekaji yameibuka upya na yanaichafua Tanzania.

Alisema kumekuwa na matukio hayo maeneo mbalimbali ambayo wakati mwingine si ya kweli na lawama zinaelekezwa serikalini na pengine vyombo vya ulinzi na usalama.

Siku tisa baadaye, yaani Julai 28, 2024, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, alikutana katika kikao cha ndani kilichohusisha taasisi zilizo chini yake, akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura. Lengo la kikao hicho lilikuwa kujadili masuala mbalimbali hususan hali ya usalama. Baada ya kikao hicho, Waziri Masauni alieleza mikakati ya kukabili vitendo huku akisema si kama vilivyokuwa vikiripotiwa kipindi hicho.

Masauni alisema kinachofanywa sasa ni kuboresha mifumo na taratibu za kukabili vitendo hivyo na siyo kutumia mbinu za kale.

Mfanyabiashara wa duka la nyama wa Lamadi, Christopher Chova, akielezea jinsi maandamano ya wananchi yalivyoanza amesema ilikuwa kama saa 2 asubuhi walionekana wanawake kama wanane wakiingia kituo cha polisi.

“Walivyofika hapa, wakaanza kudai watoto wao wawili waliopotea na hilo ni jambo ambalo linatokea mara kwa mara. Sasa wananchi wakapandwa hasira, wakavamia kituo cha polisi,” amesema Chova.

Chova anasema kumekuwa na mwendelezo wa watoto kupotea, ambapo inadaiwa Agosti 19, 2024, alipotea mtu na mdogo wake pasipojulikana. Hata hivyo, familia ya watoto hao haikuridhishwa na majibu ya polisi, ndiyo wakaamua kwenda kuuliza kinachoendelea.

“Na hilo ni jambo linalotokea mara kwa mara, wananchi wakapanda hasira kali baada ya wale wamama kufika na kuvamia kituo cha polisi… askari wote walishindwa kuvumilia kwa sababu kwenye hilo tukio na wenyewe walitaka kuuawa, ikabidi nao wajihami. Wananchi walikuwa wameshapandwa na hasira kulingana na watoto wao wanavyopotea,” anasema Chova.

Mkazi wa Busega, Neema John, anasema waliamua kuandamana kwenda kituo cha polisi ili kujua namna polisi wanavyofuatilia utekaji nyara wa watoto wao.

Anasema wamekuwa wakienda kutoa taarifa za watoto kupotea kwenye kituo hicho ili wasaidiwe, lakini askari wa kituo hicho hawafuatilii wakati wazazi wao hawajui kinachoendelea.

“Wanawake wameamua kwenda kuandamana polisi kwa sababu askari hawafuatilii, kutekwa nyara kwa watoto. Tumeandamana lakini wameamua kutufanyia vurugu na kututawanya, na wananchi wawili wamepata majeraha ya risasi na kufariki,” amedai John.

Mkazi wa Lamadi, Mahinga Lushinge, alisema matukio ya watoto kupotea yamekuwepo eneo hilo kwa muda mrefu japo yalitulia lakini yameibuka tena, ambapo siyo tu watu kupotea bali kumekuwa na taarifa wengine wanauawa.

Katika hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makanisani, Kata ya Lamadi, Mashimba Songoma, amedai “Kama siku tatu zilizopita, kumepotea kijana aliyekutwa maeneo ya Lukungu amechinjwa, amepasuliwa katikati akiwa ametolewa bandama, figo na ulimi.”

“Baada ya tukio hilo, sisi kama Lamadi tuliamua tuitishe mkutano wa hadhara wa kijiji kuyazungumzia haya, ikiwa ni pamoja na matukio mengine mbalimbali. Baada ya kutangaza mkutano huo Agosti 2, 2024, kesho yake Agosti 3 tukazuiliwa na taarifa kutoka kituo cha polisi,” amesema Songoma.

Amesema walizuiliwa wakiambiwa kuwa mkutano wanaouandaa utaleta taharuki na uvunjifu wa amani, akidai wakati wao wapo kwenye majukumu ya kiserikali ya kulinda amani kutokana na matukio yanayoendelea, likiwemo la binti wa miaka 15 akiwa na mtoto mgongoni mwenye mwaka mmoja kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

 “Wamefika pale watu wakakuta yule binti wakati anaviziwa akiwa anaingia nyumbani kwao alikabwa na kudondosha mchicha pamoja na viatu vyake, hatujui chochote kilichoendelea, kwa kuwa tulizuiliwa kufanya mkutano tukajua Mkuu wa Wilaya, OCD, mtendaji wa kata kwa kuwa walituzuia wao wawaeleze wananchi, mpaka leo hii hakuna na ndio maana wananchi wameandamana,” alisema

Baadaye jioni, Mkuu huyo wa wilaya amezungumza na waandishi wa habari akisema watu 108 wanashikiliwa na wengine wanaendelea kutafutwa kutokana na kuhusika kwao na maandamano hayo.

Amesema kuna badhi wamejeruhiwa na si kuuawa kama baadhi ya wananchi wanavyodai, huku idadi ya waliojeruhiwa itatolewa kwani bado operesheni ya kuwakamata walioandamana inaendelea.

“Kilichotokea leo kama mlivyoona ni maandamano ambayo yameleta taaruki na fujo katika wilaya yetu ya Busega na chanzo kama tulivyosikiliza wananchi wanasema ni kwa ajili ya kupotelewa watoto wawili waliopotea Agosti 19, 2024,” amesema Salim

Amesema kweli walipokea taarifa ya watoto wawili wa familia moja kupotea iliyopelekwa na wanachi katika kituo hicho cha polisi na tayari walianza kuifanyia kazi ili watoto hao wapatikane.

“Dada alikwenda kumchukua mdogo wake katika nyumba, baada ya kumtoa na kumpeleka sehemu nyingine, akapotelea hapo katikati, hajulikani alipo lakini sisi kama Serikali tunaendelea na juhudi za kumtafuta, mimi kama mkuu wa wilaya nimekuwa hapa kwa miezi takribani mitatu sijapata tukio la kupotea watoto, hili ni tukio la kwanza katika kata yetu ya Lamadi,” amesema.

Amesema pamoja na tatizo kutokea lakini wananchi hawakupaswa kuchukua hatua mikononi ikiwemo ya “kupiga mawe kamati ya ulinzi na usalama na kujaribu kuchoma moto kituo hicho cha polisi.”

“Madhara ni makubwa ni vyema kukaa chini kuongea kujua tatizo ni nini na kuchukua hatua kwa pamoja lakini kujichukulia hatua mkononi sisi kama Serikali hatuwezi kuruhusu,” amesema DC Salim na kuongeza:

“Ndio mana mmeona mabomu yamepigwa ni kwa sababu walizuia magari yote, wakaanza kuharibu miundombinu, wakaanza kuharibu maduka, kuyafungua na kuiba, lakini mabasi yaliyokuwa yanatoka Mara kupita hapa walikuwa wanayazuia na kuyavunja vioo, sasa sisi kama Serikali hatuwezi kukubali nchi hii ina utaratibu lazima tuufuate.”

Related Posts