Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WIZARA ya Nishati pamoja na Taasisi zake leo Agosti 21, 2024 zimeshiriki katika Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) yanayoendelea kwenye kijiji cha kizimkazi wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Kisiwani Zanzibar.
Katika tamasha hilo la Kizimkazi Wizara na taasisi zinatoa elimu ya utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015 pamoja na kutoa huduma kwa wananchi hususani katila utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa mwaka 2024-2034.
Katika Banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wananchi wameweza kujionea moja kwa moja shughuli za uchimbaji wa Gesi Asilia, usafirishaji na uchakataji wake kupitia teknolojia ya Uhalisia Pepe ( Virtual Reality) pamoja na kuelezwa juhudi za Serikali katika uendelezaji wa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.
Vilevile, katika banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wananchi wamejionea utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP) ambao umekuwa kivutio kikubwa kupitia kifaa cha Uhalisia Pepe, sambamba na kutoa elimu juu ya mchango wa Tanesco katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa kutoa elimu ya matumizi bora ya umeme.
Pia, Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wananchi wanapata huduma moja kwa moja za Nishati Safi ya Kupikia kupitia wadau wa usambazaji na waendelezaji wa teknolojia husika, elimu ya usambazaji umeme vijijini na vitongojini na uendelezaji wa miradi ya umeme.
Taasisi nyingine za Wizara ya Nishati zinazoshiriki Tamasha hilo ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambao wanatoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za udhibiti.
Wizara ya Nishati itakuwa na siku maalumu ya Nishati wakati wa Tamasha la kizimkazi ambapo itaendesha Kongamano la Nishati safi ya kupikia na kujumuisha wadau mbalimbali, ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Tamasha la Kizimkazi limezinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Agosti 18, 2024 ambapo kauli mbiu ya Tamasha hilo ni ‘’ Upishi Salama kwa Afya ya Mpishi na kwa Maendeleo ya Jamii’’.