AZAM FC imeanza vyema Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushinda mechi ya awali ya raundi ya kwanza nyumbani dhidi ya APR ya Rwanda kwa bao 1-0.
Kwa mashindano yanayochezwa kwa mtindo wa mtoano, huu ni ushindi muhimu sana kwa Azam, kwani unaiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele tofauti na watu wengi wanavyoamini.
Ujue kuna dhana fulani ambayo naona ya kizamani ya watu kuamini ili timu isonge mbele kwenye mechi za mtoano ambazo zina kanuni ya bao la ugenini basi inapaswa kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao nyumbani.
Ni dhana nzuri lakini kwa namna soka lilivyobadilika hivi sasa, unaweza ukapata ushindi wa idadi ndogo ya mabao nyumbani na bado ukawa na nafasi nzuri ya kusonga mbele kutokana na matokeo ya ugenini.
Naamini Azam imepata ushindi mzuri wa bao 1-0 nyumbani kwa vile wapinzani wao walitumia muda mwingi kujilinda na kuhakikisha hawafungwi idadi kubwa ya mabao na mara nyingi wakicheza soka la mabavu.
Hilo likaleta ugumu kwa Azam kupata ushindi mnono kwa vile APR waliziba vyema mianya kwa staili yao hiyo ambayo waliingia nayo Jumapili iliyopita na ilihitajika kazi ya ziada pamoja na wachezaji wabunifu ili kuwafungua.
Sasa wakiwa kwao hakuna namna watalazimika kufunguka kwa vile tayari wako nyuma kwa bao moja na matokeo ya sare au kufungwa hayatakuwa na faida kwao bali wanapaswa kushinda kuanzia mabao 2-0 au zaidi na kama matokeo yatakuwa 1-0 mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penalti.
APR wakifunguka itakuwa neema kwa Azam, kwani wataachia mianya ambayo wawakilishi wetu hao wakiitumia vyema inaweza kuwapatia mabao yatakayozidi kuwamaliza wapinzani wao.
Na hilo linawezekana kwa vile APR ni timu ambayo haina utisho au daraja la juu la kuitisha Azam hadi ishindwe kuitoa na kiukweli safari hii ikishindwa kufanya hivyo isitafute lolote la kujitetea.