Dereva wa New Force matatani kwa kuendesha mwendo kasi

Mbeya. Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, linamshikilia dereva wa basi la kampuni ya New Force (jina limehifadhiwa),  kwa kosa la kuendesha kwa mwendokasi wa zaidi ya kilomita 100 kwa saa na kukiuka sheria za usalama barabarani.

Basi hilo lilikuwa likisafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda  Tunduma mkoani Songwe kupitia barabara kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (Tanzam).

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 22, 2024, Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya (RTO), Ansigar Komba amesema dereva huyo alitenda kosa hilo Agosti 20, 2024.

“Kimsingi kosa hilo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za usalama barabarani na kuhatarisha usalama wa abiria endapo ingetokea ajali, hivyo licha ya kumshikilia, leseni yake ya udereva itafungiwa,” amesema.

Komba amesema katika kuhakikisha abiria na mali zao wanakuwa salama, wamefanya ukaguzi wa vyombo vya moto yakiwemo mabasi ya abiria na magari ya mizigo 57, kati ya hayo matano yamefungiwa kuendelea kutoa huduma hadi yafanyiwe marekebisho ya mifumo.

“Tunaendelea na operesheni ya ukaguzi wa vyombo vya moto na uwepo wa vifaa vya kisasa vya ukaguzi vinarahisisha kubaini madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, hali ambayo inahatarisha usalama wa abiria na mali zao,” amesema.

Komba amesema kama kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya,  wameweka mikakati ya kukabiliana na madereva wakorofi lengo ni kuhakikisha abiria na mali zao wanakuwa salama.

Katika hatua nyingine, ameonya madereva wa pikipiki za matairi matatu (bajaji) kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

“Kuna ajali ambazo zinasababishwa na bajaji, kuna changamoto kubwa, jiji lina bajaji zaidi ya 5,000 na bado zinaendelea kusajiliwa, hivyo ni vema sasa wakatii sheria ili kuepukana na hatari ya ajali za barabarani,” amesema.

Mkazi wa Kabwe jijini hapa, Peter Joel ameliomba Jeshi la Polisi kufanya doria nyakati za usiku ili kubaini vyombo vya moto chakavu ambavyo vinafanya safari ya kusafirisha abiria, jambo linalohatarisha usalama wa abiria na mali zao.

“Nyakati za usiku wapo madereva  wanaosababisha ajali za makusudi kutokana na kuingiza barabarani vyombo vya moto visivyo na sifa kusafirisha abiria,” amesema Peter.

Related Posts