Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameuagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya wilayani Kondoa mkoani Dodoma ili kuwarahisishia wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Hurui lililopo katika kata ya Kikore Wilaya ya Mpwapwa akiwa ziarani mkoani Dodoma.
Amewahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wengine wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Pia amewaagiza kupanda miti maeneo yote pembezoni mwa mto Hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja hilo uliowaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 ambapo daraja la awali liliharibiwa na maji.
Makamu wa Rais akiwa katika kata hiyo ya Kikore pia ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo Oktoba 30, 2024.