KIVUMBI cha Ligi Kuu Bara kitaendelea tena kesho Ijumaa kwa mchezo mmoja tu wa raundi ya pili kati ya Mashujaa itakayokuwa nyumbani kuwakaribisha maafande wenzao wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
Mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa ligi, Mashujaa ikiwa nyumbani iliondoka na pointi tatu ikiiadhibu Dodoma Jiji bao 1-0 lililowekwa kimiani na kipa wa wageni, Daniel Mgore aliyejifunga wakati akiokoa shuti la Crispin Ngushi.
Kwa upande wa Prisons ilipokuwa ugenini dhidi ya Pamba Jiji iliyopanda daraja msimu huu imelazimishwa sare ya bila kufungana, jijini Mwanza.
Mashujaa iko nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi na pointi tatu sawa na Simba inayoongoza na Singida Black Stars zikitofautiana mabao huku Prisons ikiwa nafasi ya nne na pointi moja.
Licha ya matokeo hayo, lakini msimu uliopita kila timu ilipata ushindi ugenini, Mei 20 Prisons ikiwa nyumbani iliambulia kichapo cha mabao 2-1, huku Mashujaa nayo ikipoteza kwa mabao 2-0 Uwanja wa Lake Tanganyika Desemba 08, 2023.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Bares alisema “Vijana wapo kwenye hali nzuri ya kupambana tumefanya marekebisho ya makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita na tunaamini kila mchezaji atatupa matokeo kesho.”
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata alisema “Tumeiandaa timu, tunawaheshimu wapinzani wetu haitakuwa mechi rahisi lakini tutapambana kupata pointi tatu.”