Iran yapanga kujisogeza karibu na mataifa ya Magharibi – DW – 22.08.2024

Baada ya wadhifa wake kuthibitishwa rasmi, Araghchi mwenye umri wa miaka 61, aliliambia shirika la habari la serikali ISNA kwamba wizara yake itajitahidi kukabiliana na mvutano kati yake na Marekani na pia kurejesha uhusiano na nchi za Ulaya.

Araghchi azitaka nchi za Magharibi kufufua makubaliano ya nyuklia

Hata hivyo, alitoa wito kwa nchi za Magharibi kuacha misimamo yake mikali na kuchukuwa hatua za kufufua makubaliano ya nyuklia ya Vienna ya mwaka 2015.

Araghchi aliwahi kuhudumu kama balozi nchini Finland na Japan. Baadaye, alitwikwa wadhifa wa naibu waziri wa mambo ya nje chini ya rais wa zamani Hassan Rowhani na kutekeleza jukumu muhimu katika mazungumzo ya nyuklia.

Araghchi ni kiungo muhimu cha mahusiano bora na mataifa ya Magharibi

Waziri huyo anaonekana kama kiungo muhimu wa mahusiano bora na mataifa ya Magharibi na mazungumzo ya moja kwa moja yenye umuhimu na Marekani.

Hata hivyo, wakosoaji wanatilia mashaka matarajio ya mwanadiplomasia huyo, ambaye ana uwezekano wa kuendeleza uungaji mkono wa Iran kwa makundi ya wapiganaji katika vita dhidi Israel, mpinzani wake wa muda mrefu.

Bunge la Iran laidhinisha baraza lote la mawaziri

Huku hayo yakijiri, hatua ya bunge la nchi hiyo ya Iran la kuidhinisha baraza lote la mawaziri lililopendekezwa na Rais Pezeshkian, inaadhimisha ushindi wa mapema  wa rais huyo aliyeingia madarakani baada ya ajali ya helikopta mwezi Mei iliyosababisha kifo cha mtangulizi wake .

Kikao cha bunge la Iran mnamo  Agosti 20, 2024
Bunge la IranPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Aliyepata uungwaji mkono zaidi wa wabunge ni waziri mpya wa ulinzi wa nchi hiyo, Aziz Nasirzadeh, ambaye alipata kura 281 kati ya wabunge 288 waliokuwepo. Bunge hilo lina viti 290.

Waziri wa Afya Mohammad Reza Zafarghandi alipata idadi ya chini zaidi ya uungwaji mkono kwa kura 163.

Soma pia:Rais wa Iran asema wataendelea kutoa msaada kwa Hamas

Mwanamke wa pekee aliyependekezwa katika wadhifa wa uwaziri  Farzaneh Sadegh, mwenye umri wa miaka 47, alipata kura 231 kuongoza wizara ya nyumba na barabara.

Sadegh ni waziri wa kwanza mwanamke nchiniIran kwa zaidi ya muongo mmoja.

Bunge hilo pia lilimuidhinisha waziri wa masuala ya kijasusi Ismail Khatib pamoja na waziri wa sheria Amin Hossein Rahimi wote ambao walihudumu chini ya Rais aliyefariki Ebrahim Raisi.

Bunge la Iran lina mtindo wa kuwakataa mawaziri waliopendekezwa

Kukataliwa kwa mawaziri waliopendekezwa ni suala ambalo limekuwa mtindo katika bunge la Iran, jambo linalofanya mafanikio ya Pezeshkian kuvutia zaidi.

Rais wa zamani wa mageuzi Mohammad Khatami ni rais wa pekee ambaye mabaraza yake ya mawaziri aliyoyapendekeza mwaka 1997 na 2001 yaliidhinishwa.

 

Related Posts