KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars raia wa Ubelgiji, Patrick Aussems amesema kwa sasa anajivunia upana na ubora wa timu hiyo baada ya kuanza vyema Ligi Kuu Bara msimu huu, huku wachezaji wote wakionyesha utayari wa kupambania kikosi hicho.
Aussems amezungumza hayo baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KenGold katika mechi ya kwanza iliyopigwa wikiendi iliyopita jijini Mbeya, na sasa inajiandaa na dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba.
“Tuna upana mkubwa wa kikosi jambo ambalo linatufanya sisi kama benchi la ufundi kutumia mchezaji kutokana na aina ya mpinzani tunayeenda kupambana naye katika mchezo husika, hili kwetu linatufanya kupigania malengo ya nafasi nne za juu,” alisema Aussems aliyewahi kuinoa Simba na kuongeza, licha ya uwepo wa nyota wengi wa kigeni katika timu hiyo ila kumekuwa na mwenendo mzuri kwao, huku akiweka wazi kadri wanavyozidi kucheza kwa pamoja ndivyo wanavyotengeneza muunganiko mzuri ‘Chemistry’.
Kuonyesha upana wa timu hiyo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Kengold alianza mchezaji mmoja tu mzawa, huku wengine wote wakiwa ni wageni jambo lililokuwa pia ni tofauti na mechi ya kirafiki juzi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Katika mchezo na KenGold kikosi kilichoanza kilikuwa ni; Metacha Mnata, Marouf Tchakei, Emmanuel Keyekeh, Anthony Tra Bi Tra, Joseph Guede, Ibrahim Imoro, Ande Koffi Habib Cirille, Benjamin Tanimu, Mohamed Damaro, Elvis Rupia na Josaphat Arthur Bada.
Kikosi kilichochapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar ni Ibrahim Rashid ‘Parapanda’, Edward Manyama, Kennedy Juma, Yahya Mbegu, Jimmyson Mwanuke, Khalid Habib Idd ‘Gego’, Kelvin Nashon, Najim Mussa, Ayoub Lyanga, Habib Kyombo na Hamad Majimengi.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema, nyota mpya wa timu hiyo raia wa Niger, Victorien Adebayor atawasili hapa nchini kuanzia Jumapili hii ya Agosti 25, ili kuungana na wenzake.