Kamala kutoa hotuba ya aina yake kukubali uteuzi – DW – 22.08.2024

Kamala Harris ataufunga mkutano mkuu wa Democrat kwa kukubali uteuzi huu wa kihistoria wa kuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika na Asia kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini Marekani, na kwa wengi kwenye chama chake wanangojea kuona ni jinsi gani atatumia haiba yake ya kuchangamsha, kuwashawishi mamilioni ya wapigakura ambao bado hawajaamuwa kwamba ni yeye anayefaa kumrithi Joe Biden hapo tarehe 4 Novemba.

Kamala, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, ataweka wazi maono yake juu ya Marekani anayotaka kuijenga, na wakati huo huo kujenga hoja dhidi ya mpinzani wake kutoka chama cha Republican, Donald Trump.

Soma zaidi: Biden: Okoeni demokrasia kwa kumchagua Harris

Hii itakuwa hotuba ya kuhitimisha awamu ya kwanza ya kampeni za mwezi mzima, baada ya Rais Joe Biden kuamua kujiondowa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumpendekeza makamu wake huyo kuchukuwa nafasi yake. 

Kwa mujibu wa mmoja wa maafisa kwenye timu yake ya kampeni, Kamala ana malengo matatu kwenye hotuba ya leo. Atazungumzia historia yake akiwa mtoto anayetokana na familia ya tabaka la kati, hadi kuwa kwake muendesha mashitaka, na wakati huo huo atajilinganisha na kile anachodai ni ajenda ya giza ya Trump anayetumia hamasa za uzalendo wa watu weupe kusaka kura.

Huenda pia akazungumzia siasa ya nje, hasa uungaji mkono kwa Israel na makubaliano ya kusitisha kwenye Ukanda wa Gaza.

Muelekeo mpya wa siasa?

Kamala alizungumza kwa muda mfupi siku ya Jumatatu kwenye mkutano mkuu wa chama chake, ambapo aliisifia rikodi nzuri ya Rais Biden aliyoiita ya kujivunia, na kisha siku ya Jumanne, wakati wajumbe wa Democrat walipompitisha kuwa mgombea wao wa urais.

USA |  Chicago | Kamala Harris
Kamala Harris anakabidhiwa rasmi kijiti cha kuwania urais wa Marekani.Picha: Kevin Dietsch/Getty Images

Miongoni mwa watakaozungumza kabla ya Kamala usiku wa leo ni gavana Gretchen Whitmer wa Michigan, Gavana Roy Cooper wa North Carolina, kiongozi wa vuguvugu la haki za kiraia, Al Sharpton, na rais wa chama cha walimu wa Marekani, Randi Weingarten.

Soma zaidi: Kamala Harris aashiria mabadiliko makubwa kwenye sera ya Marekani kuhusu Gaza.

Kamala Harris atakuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Afrika na Asia kukubali uteuzi wa chama kikubwa cha siasa nchini Marekani kuwania urais.

Hotuba yake ya leo inatolewa ikiwa ni siku moja tangu Gavana Tim Walz wa Minnesota kutoa hotuba yake ya kukubali uteuzi wa kuwa mgombea mwenza wa Kamala usiku wa jana.

Kwenye hotuba yake, Walz alimshukuru Kamala kwa kumuamini na kumpa uwezekano wa kuitumikia nchi yake kwenye nafasi ya juu kisiasa.
 

Related Posts