Dar es Salaam. Watoto wa marehemu Zacharia Hans Poppe, wanakusudia kuwasilisha mahakamani maombi mengine ya ama kuziunganisha kampuni tatu zinazomilikiwa na baba yao mzazi, ili ziweze kuwa sehemu ya wadaawa katika kesi ya mirathi au wachukue hatua zingine katika Mahakama nyingine.
Watoto hao, Angel na Abel ambao ni wasimamizi wa mirathi, katika kesi ya mirathi ya Zacharia Hans Poppe namba 177/2022, iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, wanakusudia kufanya hivyo, baada ya maombi yao ya awali kugonga mwamba mahakamani hapo.
Kupitia wakili wao, Emmanuel Msengezi na Regina Helman wamedai watawasilisha maombi mengine mahakamani hapo ya kuziunganisha kampuni hizo tatu ambazo ni Z.H. P Ltd, HansPoppe Hotels Ltd na Z.H.Poppe Limited ili ziwe sehemu ya wadaawa katika shauri hilo.
Amedai lengo la kufanya hivyo ni kumpa mamlaka Jaji Glady’s Nancy Barthy anayesikiliza shauri hilo, aweze kutoa amri ambazo walikuwa wameziomba ili wakurugenzi wa kampuni hizo wapeleke mahakamani taarifa za fedha pamoja na mikataba mbalimbali ya pango na mambo mengine yanayohusu kampuni hizo.
Wakili Msengezi ametoa maelezo hayo leo Alhamis Agosti 22, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi katika maombi madogo ya awali yaliyowasilishwa mahakamani hapo na watoto hao wa Zacharia Hans Poppe kupitia mawakili hao.
Katika maombi hayo, wakili Msengezi ameomba mahakama itoe amri kwa wakurugenzi watendaji wa Kampuni ya Z. H. Poppe Limited, Z.H. P Ltd na HansPoppe Hotels Ltd, ambao ni Caeser Hans Poppe na mwanawe Adam Caeser Hans Poppe, wawasilishe nyaraka mbalimbali za mikopo waliyochukua kwenye taasisi za fedha kupitia kampuni hizo mpaka sasa, taarifa ya fedha ikiwemo faida ya mwaka kwa kampuni hizo, mikataba ya kusafirisha mafuta nje ya nchi pamoja na mikataba ya upangishaji wa hoteli ya Zacharia Hans Poppe iliyopo Iringa.
Caeser ni mdogo wake, Zacharia Hans Poppe ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na Adam ni mtoto wa Caeser ambao kwa pamoja ni wakurugenzi katika kampuni ya Z. H. Poppe Ltd inayomilikiwa Zacharia kwa asilimia 90 ya hisa zote.
Hata hivyo, mahakama hiyo baada ya kupitia maombi hayo ilisema itakuwa ni vigumu kutoa amri hizo kwa kuwa kampuni hizo sio sehemu ya kesi ya mirathi iliyopo mbele yake.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Barthy amesema hawezi kutoa uamuzi dhidi ya kampuni ambayo haipo na haijaunganishwa kama sehemu ya wadaawa mahakamani hapo.
“Itakuwa ni vigumu kutoa amri hizo na uamuzi dhidi ya kampuni ambayo haipo katika shauri hili na wala haijaunganishwa kama sehemu ya wadaawa (walalamikiwa) katika shauri hili la mirathi,” amesema jaji Barthy.
“Lakini ikiwa Angel na Abel wana maslahi wanaweza kuchukua hatua zingine ikiwemo kuziunganisha kampuni hizo katika kesi hii au kwenda katika jukwaa lingine,” amesema jaji Barthy.
Kuhusu ombi la kuongeza au kupunguza orodha ya idadi ya mali za marehemu, Jaji Barthy amesema amri hiyo haijaondolewa wala kufutwa bali ipo palepale kwa ajili ya utekelezwaji.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili Msengezi ameieleza mahakama hiyo kuwa wanakusudia kuwasilisha maombi yao ya kuziunganisha kampuni hizo tatu.
“Mheshimiwa Jaji, baada ya uamuzi wako, tunakusudia kuwasilisha maombi ya kuziunganisha kampuni zote tatu zilizokuwa zinamilikiwa na marehemu Zacharia Hans Poppe ili ziweze kuwa sehemu ya wadaawa katika shauri hili ili jaji uwe na mamlaka na kampuni hizi kwa kuwa zitakuwa zimeunganishwa kama wadaawa.
Na hivyo utaweza kutoa amri ambazo tulikuwa tumeziomba za wao kuleta taarifa za fedha, mikataba mbalimbali ya pango (upangishaji) na mambo mengine,” amedai wakili Msengezi
Wakili huyo amesema:“Na kwa kuwa milango haijafungwa kwa Abel na Angel kwa kuchukua hatua zaidi ama kwenye shauri hili la mirathi au kwenye mahakama nyingineyo.
Wakiweza kuzipeleka kampuni hizi pekee bila kuhusisha na kesi hii ya mirathi wanaweza kwa sababu wana mamlaka hayo na kama wasimamizi wa mirathi ya Zacharia Hans Poppe, wanaweza kuipeleka kampuni mahakamani kumlazimisha mkurugenzi aliyopo alete vitu hivyo mahakamani,” amedai Msengezi.
Baada ya upande wa waleta maombi kutoa maelezo hayo, wakili Peter Kibatala akisaidiana na Glory Ulomi ambao wanawatetea wadaawa katika shauri hilo ambao ni Caeser na mwanae Adam Caeser, wameondoa maombi yao waliyokuwa wamewasilisha mahakamani hapo Julai 23, 2024 ya kuweka pingamizi kuwa mahakama hiyo isitoe amri kwa kampuni hizo kwa sababu hazijawekwa kuwa ni moja ya wadaawa katika shauri hilo.
“Mheshimiwa Jaji, tunaomba kuondoa maombi yetu tuliyowasilisha mahakama hapa, kwani tumeona uamuzi ulioutoa umeenda moja kwa moja kutoa amri kwa kile tulichokuwa tunaomba kwamba, mahakama yako isitoe amri yoyote dhidi ya kampuni kwani sio sehemu ya hii esi na wala haijaunganishwa kwenye kesi hii ili iweze kusikilizwa,” amedai Kibatala.
Jaji Barthy, baada ya kusikiliza hoja za pande zote alikubaliana na waleta maombi na wajibu maombi na kuahirisha kesi hadi Septemba 12, 2024 kwa ajili ya amri nyingine.
Kesi hiyo ya mirathi ya marehemu Hans Poppe, namba 177 ya mwaka 2022 imefunguliwa katika Mahakama hiyo na wasimamizi wa mirathi, wakiomba wakurugenzi wa kampuni hizo zinazomilikiwa na Zacharia Hans Poppe wawasilishe orodha ya mali zilizopo katika kampuni hizo.
Waombaji hao waliwasilisha maombi, wakiomba kusomewa orodha ya mali iliyokusanywa na kutoa taarifa ya hesabu ya fedha tangu baba yao alipofariki hadi sasa.
Vile vile wanaiomba Mahakama hiyo ielekeze wakurugenzi hao waeleze hali ya mali za marehemu Zacharia zilizopo katika kampuni zake ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi.
Zacharia Hans Poppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na maziko yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.