Bukoba. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba imelikubali ombi la Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kuzuia kutumika kwa majina na taarifa za mashahidi katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath.
Uamuzi huo wa Mahakama unatokana na maombi ya DPP kupitia maombi ya jinai namba 23143 ya 2024 ambayo yalisikilizwa chemba ili kulinda usalama wa mashahidi na ndugu zao, kwani kumekuwa na tishio la kiusalama dhidi yao.
DPP katika maombi hayo, ameeleza kumekuwepo na majaribio mbalimbali kutoka kwa washirika wa washitakiwa kupata majina na utambulisho wa watu ambao wanaweza kuwa mashahidi, kwa lengo la kuwadhuru ili wasitoe ushahidi wao.
Wajibu maombi katika maombi hayo ni Padri Elipidius Rwegashora, Novat Venant ambaye ni baba wa marehemu, Nurdin Ahamada, Ramadhan Jadius, Rwenyagira Burukadi, Danstan Burchad, Faswiu Athman, Gozbert Arikadin na Desdery Everigist.
Katika uamuzi wake alioutoa jana Jumatano Agosti 21, 2024, Jaji Gabriel Malata amezuia matumizi ya nyaraka ambazo zinaweza kutoa utambulisho wa mashahidi na nyaraka hizo, zitafanywa siri katika hatua zote za usikilizwaji wa shauri hilo.
Jaji Malata katika uamuzi wake huo, amesema usambazaji na uchapishaji wa taarifa yoyote ya ushahidi wa nyaraka na ushahidi mwingine wowote ambao utahusu utambulisho wa mashahidi wa Jamhuri hautaruhusiwa kabisa.
Si hivyo tu, lakini uchapishaji na usambazaji wa taarifa yoyote ambayo inaweza kubainisha eneo, makazi na mahali walipo mashahidi wa upande wa mashitaka au ndugu wowote wa karibu wa mashahidi hao umepigwa marufuku.
Katika uamuzi wake huo, Jaji Malata alisema usikilizwaji wa kesi hiyo utafanyika kwa faragha (held in camera) na pia kupitia video conference, matumizi ya sauti au upotovu wa uso na kutoa utambulisho wa mashahidi hautaruhusiwa.
Katika maombi hayo, DPP ameambatanisha kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kagera, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Boniface Kibuga ambaye katika kiapo hicho amejenga hoja za kuishawishi Mahakama kukubali ombi hilo.
SSP Kibuga amedai katika kiapo hicho Mei 30, 2024 akiwa katika majukumu yake, alijulishwa uwepo wa tukio lililoripotiwa huko kituo cha Polisi cha Kamachumu likihusu kuibwa kwa mtoto mwenye ualbino wa umri wa miaka miwili.
Kupitia upelelezi, amedai aligundua usiku wa Mei 30, 2024, mjibu maombi wa pili ambaye ni baba wa mzazi aliwaongoza wajibu maombi wengine ambao ndio washitakiwa katika kesi ya mauaji hadi nyumbani kwake alikokuwa akiishi.
Baada ya kufika katika nyumba hiyo, walimkuta mama wa mtoto ambaye ni mke wa Venant akiwa na mtoto wake ambapo mjibu maombi watatu, Ahamada, aligonga mlango na mama wa marehemu alifungua mlango wa nyumba yao.
Mara tu baada ya kufungua mlango, amedai mjibu maombi wa nne, Ramadhan Jadius, alimshambulia mama wa marehemu ambapo mjibu maombi wa tatu, Nurdin Ahamada, alimnyakua mtoto na kukimbia naye mahali kusikojulikana.
Katika kiapo hicho, SSP Kibuga ameeleza jitihada za kumtafuta mtoto huyo ziliendelea na Juni 17,2024, mtoto huyo alipatikana akiwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye mtaro katika kijiji cha Mulele katika wilaya ya Muleba.
Kutokana na kukusanywa kwa taarifa za kiintelijensia, RCO amedai walifanikiwa kuwakamata mjibu maombi wa tatu na wa tano wakiwa katika harakati za kuuza mifupa ambayo ilisadikiwa ilikatwa kwenye mwili wa marehemu.
Kwa kufanyia kazi maelezo ya kukiri kosa ya wajibu maombi hao ambao waliwataja wajibu maombi wengine, walifanikiwa kuwakamata wajibu maombi wengine wote na inadaiwa waliandika maelezo ya kukiri kushiriki katika mauaji hayo.
Kutokana na upelelezi na taarifa za intelijensia, SSP Kibugi anasema aliweza kubaini katika tarehe zisizojulikana Aprili 2024, wajibu maombi hao waliingia katika makubaliano haramu na kuunda genge haramu la uhalifu.
Lengo la genge hilo ilikuwa ni kuua mtu mwenye ualbino na katika kutekeleza mpango wao huo, wajibu maombi wanadaiwa kuanza kufanya vikao katika maeneo mbalimbali ya Muleba, Misenyi na Bukoba.