Tafiti nyingi zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya biashara changa na bunifu (startups) barani Afrika, changamoto yake kubwa ni kukosa mtaji na ufadhili, hili linatajwa kusababisha kifo cha zilizo nyingi bila kujali zingeleta matokeo makubwa kiasi gani.
Changamoto nyingine ni sera zisizo rafiki, usimamizi mbovu na kukosekana kwa rasilimali watu wenye uwezo wa kukuza zaidi wazo kuwa biashara, hata hivyo baadhi ya wajasiriamali wanasema ulezi na uatamizi una nafasi kubwa katika kuruka viunzi hivyo.
Ulezi na uatamizi thabiti unatajwa kuwa unatoa mwongozo na uzoefu binafsi ambao ni muhimu kwenye kujenga njia ya mafanikio, ujasiriamali na kuimarisha mustakabali, kwani inakuwa ni zaidi ya ushauri.
Miongoni mwa wabunifu wa biashara changa ni Lusekelo Nkuwi (33) ambaye amebuni aplikesheni ya Go Go ambayo inasaidia mtu kupata huduma pale anapopata dharura katika gari lake akiwa mahali ambapo ni mbali na nyumbani au na fundi aliyezoea kumhudumia.
Anasema miongoni mwa huduma zinazotolewa na Go Go ni kupata usaidizi kwa kutumia simu pindi mtu anapopata changamoto ya pancha, betri kuishiwa chaji, kuvuta gari, gari iliyojiloki pamoja na mafuta pale mtu anapoishiwa.
“Mimi nafanya shughuli za kilimo, nyumbani ni Dar es Salaam lakini nalima Morogoro, changamoto zote hizo tano nimewahi kuzipitia au watu wangu wa karibu zimepitia. Wengi wanapata changamoto hizo na hawajui cha kufanya au msaada wao uko mbali,” anasema Nkuwi.
Nkuwi anasema pamoja na kuwa suluhu hiyo ya kiteknolojia kwa muda sasa amejikita kutafuta wabia wa ndani au wa nje: “Hapa ndipo umuhimu wa uatamizi na kujengewe uwezo unapoonekana, ukishikwa mkono na watu au taasisi kubwa ni rahisi kufanikiwa.
“Ulezi na uatamizi ni kwa ajili kukuonyesha njia ya kupita, maana unapoanza na wazo ni kama kurusha jiwe gizani, wakija watu kama Vodacom wanakuonyesha mwanga na ukiwa nao baadhi ya milango iliyokuwa migumu kufunguka inaanza kulainika kuliko ukiwa mwenyewe.”
Anasema hatua aliyofikia sasa ya kushikwa mkono na Taasisi ya Mass Challenge mambo mengi yanabadilika, kwani anakutanishwa na watu na kujengewe uwezo wa namna ya kukuza biashara anayotamani kuiona ikiwa kubwa.
“Unafundishwa kujiamini, kujieleza na namna ya kufanya mazungumzo na wabia na wawekezaji watarajiwa,” anasema na kuongeza kuwa yeye na mwanzilishi mwenza wa Go Go sasa wamefanikiwa kuongeza wafanyakazi wanne.
Mwanzilishi wa Altitute X, Rose Funja naye anakubaliana na Nkuwi kuwa uatamizi ni muhimu, kwani inamfanya mvumbuzi kutuliza kichwa na kufuatilia mambo yanayoweza kumfanya asonge mbele kwa haraka, badala ya kujikuta anahangaika na kila kitu.
“Kabla ya kupata ulezi au usimamizi unajikuta unafanya kila kitu wewe, utengeneze wazo, utafute masoko, ufanye mauzo, ufanye mambo ya kitaalamu na kiutawala, lakini ukipata mtu wa kukushika mkono na kukupa mwongozo inasaidia kuruka baadhi ya vizuizi,” anasema Rose.
Anasema kupitia walezi unafundishwa namna ya kupata fedha na vitu vya kuzingatia ndiyo maana yeyote aliyepo katika ulimwengu wa uvumbuzi akipata jukwaa kama hili, ambalo unaweza kukutana na watu wakakushika mkono unachukulia kwa uzito.
“Kwa wenzetu ni utaratibu ambao umeshazoeleka na wawekezaji wanajitokeza kuunga mkono ubunifu, lakini sasa hapa kwetu siyo wengi, hivyo fursa yoyote ya kukutana na wawekezaji wa kigeni ni muhimu,” anasema.
Rose (42) anasema uvumbuzi wake unahusisha matumizi ya droni katika shughuli za kilimo na ukusanyaji wa taarifa muhimu kwa ajili ya kushughulikia masuala mtambuka katika jamii, kama vile mawasiliano na nishati.
Anasema msingi wa uvumbuzi huo ni changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo nchini, lakini pia umuhimu wa picha na taarifa za anga kwa ajili ya kusaidia uchukuaji wa hatua.
“Kilimo ni sekta muhimu, lakini hivi karibuni imekabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na watu wanashindwa kutumia taarifa zilizopo kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi, kupitia ubunifu wetu tunatoa suluhu.”
Vilevile Rose anasema mbali na kukusanya taarifa, droni hizo ambazo kila moja inakuwa na uzito wa walau kilo 50, zinatumika kunyunyizia viuatilifu na mbolea kwenye mashamba kwa usahihi mkubwa, hivyo kila eneo linafikiwa.
Rose, ambaye hivi sasa ana droni ambazo anahitaji kuzihamisha kila anapotaka kutoa huduma, yeye na mwanzilishi mwenza wanahitaji Dola 500,000 (Sh1.35 bilioni) kwa ajili ya kukuza wigo wake wa huduma katika maeneo ya kimkakati.
“Kitu ninachokifanya kinahitaji fedha nyingi, droni moja ni Dola 30,000 (Sh81.2 milioni), lakini kunahitajika jenereta kwa kuwa betri hazikai na chaji muda mrefu, lakini pia vyote hivyo vinahitaji usafiri, maana droni na jenereta vyote vinapima kilo 100,” anasema Rose, ambaye naye atashiriki safari ya Mass Challenge nchini Marekani.
Frank Mussa (24) ambaye ameanzisha Mkanda salama ambao ni kifaa kinachosaidia kuzuia kutoka kwa damu wakinamama baada ya kujifungua, anasema kifaa hiki ni rahisi kutumia, lakini pia ni bei nafuu na hakina madhara yoyote kwenye mwili wa mama baada ya kujifungua, anasema bila ulezi ni vigumu kupata mafanikio.
“Acceleration na proper mentorship (ulezi) zina mchango mkubwa katika kukuza bunifu kwenye sekta zote, kwanza inasaidia kutengeneza msingi mzuri wa kibiashara (innovation commercialization) na inasaidia wabunifu kujua na kupata fursa mbalimbali, hasa za uwekezaji (investment opportunities).”
Anaongeza kuwa faida nyingine ya ulezi na uatamizi ni kupata mwongozo sahihi wa kuendesha biashara. Acceleration programu kama ya Vodacom ina mchango mkubwa kwa wabunifu wenye bunifu zinazotatua changamoto kwenye jamii
“Lakini wabunifu wengi wanakosa fursa hiyo na nyinginezo kwa sababu, hawapo tayari kuzitafuta, lakini pia bunifu nyingi bado zipo kwenye ideation, ni jukumu la mbunifu kutoa ubunifu wake kwenye ideation stage (wazo) na kuiweka kwenye prototyping stage (bunifu kifani) ili aweze kupata kushikwa mkono na wadau mbalimbali,” anasema Mussa.
Mwanzilishi huyo wa Afya Lead anasema safari yake ya Marekani inayotarajiwa Oktoba mwaka huu, ni fursa muhimu sana kwake, kwani inaweza kumfanya apige hatua kwenye ubunifu.
“Bila shaka nitapata nafasi ya kukutana na mentors (walezi) wangu waliopo Boston, lakini pia nitapata nafasi ya kujifunza vitu vipya, hasa kutoka kwa wabobezi wa Mass Challenge na muhimu zaidi nitapata fursa ya kutangaza kazi ninayofanya kuimarisha huduma za afya nchini kwetu.”
Anasema mwanzo wa wazo lake ni baada ya kuona utokaji wa damu nyingi ndicho chanzo cha vifo vya wajawazito wengi nchini Tanzania, ambapo asilimia 29% ya vifo vya wakinamama vinatokana na utokaji wa damu nyingi baada ya kujifungua.
Aidha miongoni mwa kampuni ambazo zinafanya ulezi kwa wabunifu wachanga ni Kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia programu ya Vodacom Digital Accelerator, ambayo husaidia kuanzia awali ubunifu wa kiteknolojia ambao unaweza kuuzika sokoni.
Programu hiyo huwachukua waanzilishi na kuwapatia mafunzo ya kitaalamu, ushauri na usaidizi wa kiufundi, pia inatoka fursa ya kutumia zana mbalimbali na ufadhili ambao unawezesha kukua na kuwa biashara inayoweza kuleta faida.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire anasema programu hiyo inasaidia maono ya wanaoanza kwa kuwapa waanzilishi uhuru kamili na udhibiti wa ramani ya uanzishaji wao. Pia inalenga kuhamasisha na kufuatilia kwa haraka uwezo wa waanzilishi wa uanzishaji wa kuzalisha vianzio endelevu kupitia shughuli za kuongeza kasi na za kimwili na uthibitishaji.
“Mfumo wa ubunifu Tanzania uko tayari kwa ukuaji. Mwaka huu pekee, tulipokea zaidi ya maombi 200 na tumeweza kufanya kazi na 20 na mwishowe wakabakia saba kisha watatu. Niwaalike kampuni, wawekezaji na wabia kuchangamkia soko la Tanzania, kuna watu wenye akili timamu ambao wanahitaji tu kuimarishwa”