Mahakama yazuia tangazo la kufutwa vijiji lililotolewa na Serikali

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imezuia tamko la Serikali namba  673 la Agosti 2, 2024 la kufuta kata, vijiji na vitongoji, vikiwamo vya wilayani Ngorongoro, hadi amri ya Mahakama itakavyoelekeza vinginevyo.

Uamuzi huo ulitolewa jana  na Jaji Ayoub Mwenda, aliyesikiliza maombi madogo ya zuio hilo yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Posi, kupitia wakili Peter Njau.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mwenda aliridhia maombi hayo madogo na kukubali zuio la kusimama tamko hilo kupisha usikilizaji wa maombi ya msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha, wakili Njau amesema katika maombi hayo madogo namba 6953 ya mwaka 2024, wameyawasilisha mahakamani jana, kusikilizwa na kutolewa uamuzi huo.

Amesema maombi hayo madogo yalikuwa na hoja mbili, ya kwanza ni kuomba zuio hilo na ya pili ambayo ni kuu katika shauri hilo ni kuiomba mahakama itoe kibali cha mleta maombi  kufungua maombi ya marejeo ya amri hiyo kama ilikuwa halali au laa.

“Jaji ameridhia maombi yetu na ametuamuru tuwape nakala za maombi yetu upande wa Jamhuri (mjibu maombi) kwa hiyo amri ile ya tangazo la Serikali itasimama ili kupisha maombi mama kama amri ile ilikuwa halali au laa,” amesema.

“Mteja wangu na wengine ambao ni wakazi wa Ngorongoro wanahisi aliyetoa amri ile hakuwa na mamlaka stahiki kuitoa na haikutolewa kihalali, hivyo kwenye maombi ya msingi mahakama itatazama hilo,” amesema.

Jaji Mwenda ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 26, 2024 mahakama itakaposikiliza maombi ya msingi ya Ole Posi.

Agosti 2, mwaka huu lilitolewa tangazo la Serikali chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za wilaya, ilitoa tamko la kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.

Related Posts