MAKAMU WA RAIS AHITIMISHA ZIARA YA KIKAZI MKOANI DODOMA – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Madini kusimamia kwa uangalifu uvunaji wa madini ya kimkakati yanayopatikana mkoani Dodoma ili yaweze kuwanufaisha wananchi wa mkoa huo.

 

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi akiwa katika Kijiji cha Mpwayungu Jimbo la Mvumi wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku nne mkoani.

 

 

Amesema Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na madini ya kimkakati mengi zaidi kuliko mikoa mingine hivyo ni fursa kwa wananchi wa mkoa huo kupiga hatua za maendeleo.

 

 

Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo mkoani humo ikiwemo kuanza kilimo cha mazao mapya ambayo yanastawi mkoani humo kama vile parachichi, maembe, mitende, komamanga, mizeituni pamoja na karanga miti.

 

 

 

Pia amesema bado fursa ipo katika kuongeza wigo wa kilimo cha mazao ya kimkakati kama vile kilimo cha alizeti, mpunga, mbogamboga pamoja na zabibu. Amewasihi wananchi wa Dodoma kuchangamkia fursa za ufugaji wa wanyama na samaki kwa njia za kisasa zaidi.

 

 

Makamu wa Rais amesema kipato cha mwananchi wa kawaida mkoani Dodoma bado ni kidogo na hakilingani na fursa zilizopo. Amewataka viongozi wa mkoa wa Dodoma kufanya juhudi kuhakikisha fursa zilizopo zinawanufaisha wananchi na kuongeza mchango wa mkoa huo katika pato la Taifa.

 

 

 

Halikadhalika amesema bado hali ya utunzaji mazingira hairidhishi mkoani Dodoma ambapo ametoa wito wa kuongezwa juhudi katika kulinda mazingira, kutengeneza mashamba ya miti, bustani za kupumzika, bustani za miti dawa, kulinda misitu ya asili, kulinda ardhi oevu ili kuweza kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kulinda vyanzo vya maji.

 

 

 

Akizungumzia tatizo la uvamizi wa tembo katika vijiji vya mvumi, Makamu wa Rais ameagiza kuongezwa vituo vya kudhibiti tembo pamoja na nguvukazi ya doria za mara kwa mara ili kudhibiti Tembo hao kuendelea kuleta madhara.

 

 

Pia ameiagiza Wizara ya Kilimo kujenga miundombinu ya kuzuia tembo katika mradi wa wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mlazo/ Ndogowe iliyopo katika Kijiji cha Mlazo ili mazao yatakayozalishwa yasiharibiwe na tembo hao.

 

 

 

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara nchini (TANROADS) kuhudumia barabara ya Mpunguzi – Mlazo yenye urefu wa kilometa 84 kwa kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa mradi mkubwa wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) wa Skimu ya Umwagiliaji ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mlazo/ Ndogowe pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 

 

 

Awali Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mhe. Livingstone Lusinde ameipongeza Serikali kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo hilo na kutoa ombi la kudhibitiwa kwa Tembo ambao wamekua wakiharibu mazao, mali pamoja na kukatisha uhai wa baadhi ya wananchi.

 

 

Makamu wa Rais amehitimisha ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Dodoma ambapo ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Related Posts