Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameitaka Serikali kukaa chini na wakazi wa Ngorongoro, na kuona namna ya kumaliza changamoto zilizopo eneo hilo badala ya kutumika kwa nguvu.
Mbali na hilo, Mbowe amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kama ‘mfariji mkuu’ kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro pamoja na kuwarejeshea huduma za kijamii.
Mbowe ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 22, 2024, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Msingi wa hoja ya Mbowe ni maandamano yanayoendelea ya baadhi ya wakazi wa hifadhi ya Ngorongoro, wanaopinga kinachotajwa kufutwa kwa vijiji vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.
Katika maelezo yake, Mbowe amesema: “Rais Samia akiwa mfariji mkuu, atumie mamlaka yake kurejesha haki za raia kwa wananchi wa Ngorongoro.”
Amedai kuna tangazo la kufuta kata, vijiji na vitongoji Ngorongoro, hivyo wao chama wanapinga hatua hiyo na wanaungana na wengine wote wanaopinga hilo.
Hata hivyo, Jumapili Agosti 18, 2024, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kupitia taarifa kwa umma, ilisema hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na shughuli za utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea kama kawaida.
“Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa, kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi.
“Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari za kuja Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi,”ilisema na kuongeza taarifa hiyo.