Mikoa mguu sawa, Riadha Taifa ikifunguliwa leo

Mikoa imetambiana kutwaa ubingwa wa riadha kwenye mashindano ya Taifa yanayofunguliwa kesho Ijumaa jijini hapa.

Tayari mikoa karibu yote imewasili jijini Mwanza tayari kwa mashindano hayo ya siku mbili yatakayofikia tamati keshokutwa Jumamosi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa baadhi ya mikoa wameeleza walivyojipanga kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Kocha wa mkoa Pwani, Elias Hotay amesema timu yao yenye wachezaji 10 na viongozi wawili imejipanga kwa ushindi na kuendeleza rekodi yao ya kufanya vizuri.

Japo amekiri kukabiliana na upinzani kutoka kwenye mikoa ya Zanzibar kwa ukanda wa Pwani na ile ya Arusha na jirani zao Dar es Salaam.

“Tutachuana kurusha kisahani na kuruka juu na kuruka chini sanjari na mbio za mita 100, 200, 400 na 800,” amesema.

Hotay amewataja baadhi ya wanariadha watakao uwakilisha Pwani ni; Benedictor Mathias, Baraka Paul, Enos Mushi, Sullei Kombo, Siwema Julius, Gaudencia Maneno na Shija Bernard.

Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam, Samwel Mwera amesema wanakwenda kupambana. 

Dar es Salaam yenye wanariadha 10 na viongozi wawili itachuana kwenye mbio fupi na za kati katika mashindano hayo.

Mwera nyota wa zamani wa Afrika wa mbio za mita 800 amesema, lengo lao ni kurudi na ubingwa. 

“Kila mkoa umejipanga, tunajua ugumu wa mashindano ya taifa, hivyo tuko mguu sawa kwa upinzani,” amesema Mwera. 

 Mwenyekiti wa Riadha Arusha, Gerald Babu ametamba hakuna wa kuwaondoa kwenye ramani ya ubingwa. 

Amesema, kama mkoa wa Mjini Magharibi wa visiwani Zanzibar utakuwepo kwenye mashindano hayo ndio utawasumbua, lakini bado hautaizuia Arusha kuendeleza rekodi ya ubingwa.

“Mkoa wa Pwani nao utatusumbua sumbua kwenye mbio fupi, lakini michezo mingine iliyosalia Arusha ni bingwa,” amejinasibu Babu.

Mikoa mingine inayotarajiwa kutoa ushindani ni wenyeji Mwanza, Mara, Morogoro, Manyara na mikoa ya Visiwani Zanzibar ambayo imekuwa ikitamba pia kwenye mitupo na mbio fupi.

Akizungumzia mashindano hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Jackson Ndaweka amesema maandalizi yamekamilika yatafunguliwa  yakiongozwa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo watakaoambatana na Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Silas Isangi.

Amesema karibu mikoa yote imekwishawasili jijini Mwanza tayari kwa mashindano hayo yatakayishirikisha wanariadha wa miruko, mitupo na mbio za uwanjani.

Related Posts