Minziro aibukia Mwadui FC | Mwanaspoti

BAADA ya kuachana na Kagera Sugar, Fredy Felix ‘Minziro’ ameibukia Mwadui FC inayojiandaa na Ligi ya Champpionship msimu huu, huku akipewa kibarua cha kuunda kikosi cha timu hiyo kitakacholeta ushindani na kupanda Ligi Kuu.

Minziro aliachana na Kagera Sugar baada ya mkataba wake kuisha msimu uliopita nafasi yake ikichukuliwa na Mganda, Paul Nkata, ambapo ameingia makubaliano ambayo hayajawekwa wazi na Mwadui akichukua nafasi ya Salhina Mjengwa aliyeipandisha daraja.

Mmoja wa viongozi wa Mwadui, Waziri Gao aliliambia Mwanaspoti kwamba kwa sasa hawawezi kuweka wazi kila kitu kinachoendelea huku wakiomba takribani siku 10 mambo yakamilike na wataweka bayana kila kitu kinachoendelea kwenye klabu yao.

“Tumempata mwalimu ni Minziro bado anatengeneza timu yake hatuwezi kuzungumza kwa sasahivi mpaka mambo yakamilike, kwa sasa hakuna jipya bado tunajiandaa,” alisema Gao na kuongeza;

“Nadhani tutakuwa na cha kuzungumza baada ya siku 10 mwalimu akishatengeneza timu yake tutakuwa na msemaji na idara mbalimbali hapo sasa mtakuwa na watu ambao mnaweza kuwafikia na kuzungumza na timu muda wote.”

“Kwa sasa hivi hakuna kilichokamilika kila kitu kinaandaliwa kuhusu timu bado tuko vitani tunaendelea kutengeneza timu kocha ndiyo kafika anaunda timu yake kwahiyo mtupe muda tutawajulisha kinachoendelea,” aliongeza.

Kwa upande wake, Felix Minziro alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema kwa sasa hana cha kusema hivyo watafutwe viongozi wa Mwadui ambao ndiyo wanajua nini kinachoendelea.

Related Posts