WAPO Watanzania wengi ambao wakiulizwa waonyeshe taifa la Cameroon lilipo katika ramani ya Afrika wanaweza kushindwa mtihani.
Ukiondoa rekodi ya kuwa taifa lililoongozwa na Rais mmoja, Paul Biya kwa miaka mingi, Cameroon haiko sana katika vichwa vya habari za kisiasa.
Jambo kubwa na la pekee ambalo limeitangaza Cameroon kwenye vichwa vya habari kwa miaka mingi ni mpira wa miguu.
Utamuongelea Roger Milla, Thomas N’kono, Emmanuel Kunde, Ebelle ‘Eugène’ Ekéké, Cyrille Thomas Makanaky na timu yao ya Simba Wasioshindwa (Indomitable Lions). Utamuongelea Samuel Eto’o wa Barcelona na Andre Onana wa Manchester United, utamuongelea Che Fondoh Malone na Willy Essomba Onana wa Simba.
Jina moja kutoka Cameroon linalosimama peke yake si jingine bali ni la Issa Hayatou ambaye aliaga dunia wiki iliyopita ikiwa ni mkesha wa kuamkia kutimiza umri wa miaka 78.
Hayatou alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi kuanzia nyumbani kwao Cameroon hadi Urais wa Fifa ambao aliukaimu kati ya mwaka 2016 na 2017.
Hayati Hayatou pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kwa miaka 15 kati ya 2001 hadi 2016 na baadae kuwa Mjumbe wa Heshima (Honorary member) baada ya kustaafu.
Issa Hayatou alizaliwa Agosti 9, 1946 katika koloni la Ufaransa la Cameroon akiwa ni mtoto wa Sultan wa kimila.
Hayatou alikuwa bingwa wa taifa wa mbio za kati yaani mita 400 na mita 800 kuanzia mwaka 1964 hadi 1971.
Alicheza kwenye timu ya taifa ya mpira wa kikapu na ya soka ya Chuo Kikuu kabla ya kukwea katika uongozi wa chama cha soka cha Cameroon 1986. Kabla ya hapo alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka akiwa chini ya wizara ya vijana na michezo.
Miaka miwili baada ya kuongoza Fecafoot akagombea na kushinda nafasi ya juu ya mpira wa Afrika yaani urais wa CAF katika uchaguzi uliofanyika Morocco 1988.
Urais wa CAF ulimpa nafasi Hayatou ya kuuendeleza mpira wa Afrika kwa kujenga mahusiano ya karibu na Shirikisho la Vyama vya Soka vya Ulaya (UEFA) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Kupitia mahusiano hayo CAF na vyama vya mpira vya Afrika vikafaidika na miradi mbalimbali ya kuendeleza mpira wa miguu.
Ni vigumu kuongelea maendeleo ya mpira wa miguu Afrika bila kumtaja yeye. Unapoitaja CAF ni kama unamtaja gwiji huyo aliyeuongoza mpira wa Afrika kwa miaka 29.
Mwaka 1988 Cameroon iliweza kuchukua Kombe la Afcon lakini ikaja kuweka alama katika historia ya mpira pale mwaka 1990 ilipofanikiwa kuwa timu ya kwanza Afrika kuingia robo fainali ya Kombe la Dunia.
Hayatou aliyatumia mafanikio haya kuweka msukumo kwa Fifa ili Afrika iongezewe nafasi katika Kombe la Dunia na kweli akafanikiwa kwa Afrika kupata nafasi 5 kutoka mbili za awali.
Mwaka 2010 Issa Hayatou alifanikisha kuleta mashindano ya Kombe la Dunia barani Afrika. Hii ilitokana na mahusiano yake mazuri na mpinzani wake katika uchaguzi wa rais wa Fifa wa mwaka 2002, Joseph Blatter na pia juhudi za Nelson Mandela.
Afrika Kusini iliyaandaa kwa mafanikio mashindano haya, pengine kwa ubora kuliko mataifa ya Ulaya yaliyokuwa na wasiwasi kuhusu Afrika kuandaa mashindano makubwa kabisa ya soka ulimwenguni.
Ni mlolongo mrefu wa mafanikio ambayo mpira wa Afrika na Dunia ulipata katika miongo karibu mitatu ya utawala wa Hayatou.
Mambo mengi yamefanyika kama kuongeza mashindano, kufundisha wataalamu wa michezo na zaidi kuongeza mapato ya CAF zikiwemo fedha za maendeleo na udhamini wa mashindano.
Mwaka 2015 na 2016 Issa Hayatou alikuwa Kaimu Rais wa Fifa wakati rais wa wakati huo Sepp Blatter aliposimamishwa kutokana na kashfa za kimaadili.
Issa Hayatou, labda kwa kuwa alikuwa na asili ya kichifu, hakuwa mtu wa maneno mengi ila matokeo ya kazi zake yalionekana. Aliwashughulikia kibabe wapinzani wake kisiasa na kwa nguvu hiyo aliweza kudumu katika ofisi kwa miaka inayokaribia umri wa kustaafu mcheza kandanda.
Issa Hayatou alizijua fitina za mpira wa Afrika na mpira wa dunia kwa ujumla. Hata hivyo, nguvu za Hayatou zilikuja kukwaa kisiki kupitia ujio wa rais wa sasa wa FIFA yaani Giani Infantino.
Inasemekana Infantino aliongoza fitina ya kuhakikisha Hayatou ambaye alikuwa pia mmoja wa makamu wa Rais wa Fifa anang’olewa katika uchaguzi uliofanyika Addis Ababa, Machi 2017.
Kwa hapa nyumbani,ni kipindi cha Issa Hayatou Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kilipopewa nafasi ya mwanachama mshiriki (Associate member) wa CAF na matokeo yake ni Zanzibar kuendelea kuwakilishwa kwenye mahindano ya klabu barani Afrika.
Pia katika mkutano uliomg’oa yeye ofisini, Hayatou alikuwa amemaliza kusimamia kura iliyoipa ZFA uanachama kamili (full membership) wa CAF. Hata hivyo, uanachama wa Zanzibar ulikuja kufutwa miezi michache baadae na Kamati ya Utendaji ya CAF iliyoketi Morocco chini ya mrithi wa Hayatou, yaani Hamad Hamad.
Alikuwa ni Hayatou aliyeishauri Tanzania kuandaa mashindano ya vijana ya Afcon chini ya miaka 17 ya mwaka 2019. Hii ilikuwa baada ya serikali ya Tanzania chini ya Rais Jakaya Kikwete kuomba na kukosa nafasi ya kuandaa Afcon ya mwaka 2017 baada ya Libya iliyokuwa iwe mwenyeji kujitoa baada ya kkabiliwa na changamoto za usalama.
Tanzania ilikosa sifa kwani haikuwa na uzoefu wa kuandaa mashindano makubwa ya Afrika hivyo mashindano yakaenda Gabon. Ni baada ya kuandaa mashindano ya U-17 ya mwaka 2019, Tanzania na Afrika ya Mashariki imepata kigezo cha uzoefu hivyo kupewa nafasi ya kuandaa mashindano ya Afcon kwa pamoja mwaka 2027.
Inahitaji jarida kubwa kuandika wasifu wa Issa Hayatou kama mtu binafsi, mwanamichezo na mtawala. Itoshe kusema amepoteza shindano lake dhidi ya matatizo ya figo na kuangushwa na kifo katika jiji la Paris, mahali na wakati wa mashindano ya Olimpiki ya 2024. Hayatou ametumika na kuweka alama kama mwanamichezo na mjumbe wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki.
Nenda salama, pumzika kwa amani Wafaranasa wanasema ‘Hommage a Issa Hayatou’. Pumzika Baba wa Soka Afrika.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.