USHINDANI mkali wa timu zinazotafuta nafasi ya kucheza hatua ya nane bora katika ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL), umeonyesha timu nne ndizo zenye nafasi kucheza hatua ya nane bora.
Hatua ya nane bora itatokana na timu zilizofanya vyema baada ya kila moja kumaliza kucheza michezo 30.
Timu zilizojiweka katika nafasi ya kufuzu ushiriki wa hatua hiyo ni Dar City yenye pointi 46, UDSM Outsiders (46), Savio (44) na JKT (39).
Dar City, UDSM na Savio kila moja imebakiza michezo 6 kumaliza mzunguko wa pili huku timu ya JKT ikibakiza michezo 8.
Timu nne zinazofuatia ni Mchenga Stars yenye pointi 38, Vijana ‘City Bulls’€pointi 37, ABC (34) na DB Oratory (33) zinaweza zikashushwa endapo zitapoteza baadhi ya michezo ambayo zimebakisha kumaliza msunguko wa pili wa ligi hiyo.
Mchenga Stars imebakiza michezo minane, Vijana ‘City Bulls’ imebakiza michezo 6, ABC (michezo 10) na DB Oratory mitano.
Timu zilizoonekana kuwa na kiu kubwa ya kuzishusha timu hizo ni Srelio yeye pointi 33, Pazi yenye 30 na Mgulani JKT 29.
Kwa upande wa timu hizo, Mgulani JKT iliyoanza kucheza na vigogo wa ligi ya kikapu na kushinda imebakiza michezo 9, Pazi michezo 7 na Srelio 6.
Mfumo utakaotumika katika hatua ya nane bora ni mshindi wa kwanza kucheza dhidi ya wa nane, 2 vs 7, 3 vs 6 na 4 vs 5.