Nsekela afafanua ujenzi kituo cha Suluhu Sports Academy

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kituo cha Suluhu Sports Academy kinachojengwa kitakuwa kitovu cha michezo mbalimbali.

Nsekela ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho, ameyasema hayo Zanzibar leo, Agosti 22,2024 kwenye hafla ya kuweka jiwe la msingi katika akademi hiyo inayojengwa Mkunguni- Kizimkazi Zanzibar huku mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

“Hii ni awamu ya kwanza ya kujenga kiwanja kikubwa cha mpira chenye uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 na kitakidhi vigezo vyote vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa hiyo kama wadau tunajivunia kwa wazo hili,” amesema.

Nsekela ametaja mambo mengine yanayotarajiwa kuambatana na kituo hicho kuwa ni kiwanja cha mpira wa pete, mpira wa kikapu, bwawa la kuogelea lenye vigezo vya Olimpiki, mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza watu 92.

“Kutakuwa na jengo la utawala lenye ofisi 10, kwa kuzingatia imani ya wananchi wa Kizmkazi eneo hili kutakuwa na msikiti wa kuchukua watu 150, kutakuwa na madarasa mawili yatakayotumika kufundishia elimu ya mpira, fedha na ujasiriamali,” amesema Nsekela.

Katika maelezo yake Nsekela amebainisha kutakuwa na nyumba nane kwa ajili ya wakufunzi mbalimbali na kwa kuzingatia mazingira ya kibiashara kutakuwa na  duka kubwa (Shopping Mall).

“Kutakuwa na gym, vilevile kutakuwa na ukumbi wa mikutano wa watu zaidi ya 500,” amesema Nsekela.

Kuhusu ujenzi wa mradi wa kiwanja hicho

Nsekela amesema kituo hicho kinajengwa kwa fedha zinazochangwa na wadau wa maendeleo, mkandarasi anayejenga mradi huo ni mzawa pamoja na wahandishi wake na hata wanaotoa huduma zinazohitaji katika ujenzi huo kama saruji, nondo ni Watanzania.

Nsekela amesema hadi sasa wameshatoa ajira za kudumu kwa Watanzania 250 lakini ajira za muda mfupi ni nyingi na wakazi wa eneo hilo wananufaika katika upikaji wa chakula na utoaji wa huduma nyingine katika kukuza uchumi wao.

“Tutajenga mradi wa kupata maji safi lakini tunaimani kujenga kituo hiki watapatikana vijana wengi wenye vipaji vya kucheza soka kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga,” amesema.

Related Posts