Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu raia 32 wa Malawi kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi mitatu kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kuwepo nchini Tanzania bila kuwa na kibali.
Pia mahakama hiyo, imeelekeza washtakiwa hao baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo, warejeshwe nchini kwao kila mmoja.
Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kulipa faini na hivyo watakwenda kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi, Agosti 22, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwakuga baada ya kukiri shtaka hilo na kutiwa hatiani.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mwakungu amesema kosa linalowakabili washtakiwa hao lina adhabu ya kifungo au faini au Mahakama inaweza kutoa adhabu zote kwa pamoja.
Amesema washtakiwa wametiwa hatiani kwa mujibu wa sheria kama walivyoshtakiwa baada ya kukiri shtaka lao na hivyo mahakama hiyo inawahukumu kulipa faini ya Sh 500,000 au kutimikia kifungo cha miezi mitatu jela kwa kila mmoja.
“Mahakama imetoa adhabu hiyo kwa kuzingatia washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, wamekiri mashtaka yao bila kuisumbua Mahakama na wameomba msamaha wa wa dhati mahakamani hapa,” amesema Hakimu Mwankuga.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, washtakiwa walipewa nafasi na mahakama hiyo ya kujitetea kwa nini wasipewe adhabu kali na utetezi wa baadhi yao ulikuwa kama ifuatavyo:
Mshtakiwa Magreth Mwenda ameomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto watano wanoamtegemea na wazazi wake wote wawili walishafariki.
Mshtakiwa Brenda Banda yeye amedai yupo Tanzania kimakosa hivyo anaomba apunguziwe adhabu kwa sababu ana watoto wawili wanaomtegemea ambao amewaachia majirani.
Kwa upande wake, mshtakiwa Edwin Pili yeye amedai kuwa alikuja Tanzania kutafuta maisha na kwamba hajaja kwa ubaya.
Mshtakiwa Mika Emanuel ameomba apunguziwe adhabu kwa sababu amekamatwa na mke wake na kwamba wana watoto wawili wanaowategemea.
Kwa upande wake, Daudi Phiri yeye aliomba mahakama impe nafuu na impunguzie adhabu kwa sababu mke wake ana ujauzito wa miezi tisa.
Baada ya kumaliza kujitetea, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa kutoka ofisi ya Uhamiaji, Raphael Mpuya akishirikiana na Ezekie Kibona, wameiomba mahakama itoa adhabu kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Mwakuga baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili amewahukumu washtakiwa hao kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kila mmoja na wakishindwa kulipa faini basi watatumikia kifungo cha miezi mitatu jela.
Awali, baadhi ya washtakiwa walidai hawajui lugha ya Kiswahili wala Kingereza bali wanajua lugha ya Chichewe.
Hali hiyo ilisababisha mahakama kutafuta mkalimani wa lugha aitwaye Whatson Kaunda (60) ambaye alitafsiri kutoka lugha ya washtakiwa hao ambayo ni Chichewe kwenda lugha ya Kiswahili.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Agosti 20, 2024, eneo la Msasani Bonde la Mpunga, lililopo Wilaya ya Kinondoni, wakiwa raia wa Malawi, walikutwa wakiwa nchini Tanzania bila kuwa na hati ya kusafiria au nyaraka yoyote inayoonyesha uhalali wa wao kuishi nchini.