Somalia yatishia kusitisha safari za ndege za Ethiopia – DW – 22.08.2024

SCAA imesema Shirika hilo la Ndege la Ethiopia linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo, halijashughulikia malalamiko ya awali kuhusu maswala ya uhuru na kwamba pia linaondoa majina ya maeneo zinazoelekea ndege nchini Somalia na kubakiza tu nambari za viwanja vya ndege.

Katika barua iliyochapishwa na shirika la habari la serikali ya Somalia, SCAA imesema hatua hiyo inazidisha wasiwasi wa awali na kudhoofisha uhuru wa Somalia.

Somalia yatishia kuchukuwa hatua kufikia Agosti 23

Barua hiyo imeendelea kusema iwapo masuala hayo hayatatatuliwa ifikapo Agosti 23, mamlaka hiyo haitakuwa na budi ila kusimamisha safari zote za ndege za Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Somalia, kuanzia tarehe hiyo.

Soma pia;Mazungumzo ya Somalia, Ethiopia yamalizika bila makubaliano

SCAA imeongeza kwamba kujirudia tena kwa hali ya kutotambulisha vyema maeneo zinapoelekea ndege nchini Somalia, kutasababisha kusimamishwa kwa safari hizo bila onyo zaidi.

Raia wa Somalia walalamika kuhusu safari za ndege za Ethiopia 

Pia katika barua hiyo SCAA imesema imepokea idadi inayoongezeka ya malalamiko yasiyokubalika kutoka kwa raia wa Somalia kuhusu matukio wanayokumbana nayo kwa kusafiri na ndege za Shirika la Ndege la Ethiopia.

Picha ya hargeisa, mji mkuu wa Somaliland, iliyochukuliwa Aprili 2024
Mji wa hargeisa, SomalilandPicha: Eshete Bekele/DW

Kwasasa, tovuti ya shirika hilo la ndege, inaorodhesha mji mkuu wa Somaliland Hargeisa bila kutaja nchi na utafutaji wa Somaliland hauonyeshi maeneo zinapoelekea Ndege.

Utafutaji wa Mogadishu unabainisha wazi kuwa mji huo uko Somalia.

Somalia pia yaiandikia barua Fly Dubai

Barua tofauti, ambayo pia ilichapishwa na shirika hilo la habari la serikali ilitumwa kwa shirika la ndege la Fly Dubai linalomilikiwa na serikali ya Imarati.

Barua hiyo ilisema shirika hilo lazima lishughulikie ukiukaji mkubwa na kutaja bayana maeneo ya safari zake za ndege ndani ya Somalia katika huduma zake za tiketi .

Soma pia:Nchi hasimu za Somalia na Ethiopia zafanya mazungumzo Uturuki

Kwasasa , tovuti ya kampuni hiyo inaorodhesha jiji la Hargeisa huko Somaliland. Fly Dubai ilisitisha safari zake za Mogadishu mwezi Juni kutokana na masuala ya usalama.

SCAA imesema kushindwa kutimiza masharti hayo kufikia Agosti 24 kutasababisha kufutiliwa mbali mara moja kwa kibali cha safari za ndege za Fly Dubai ndani ya Somalia.

Soma pia:Somalia yamfukuza balozi wa Ethiopia

Barua hizo zinakuja kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Somalia na Ethiopia, yaliyoratibiwa na Uturuki, ambayo mapema mwezi huu, waziri wake wa mambo ya nje Hakan Fidan aliyataja kuwa maendeleo makubwa.

Ndege za Shirika la ndege la Ethiopia zinasafiri hadi mji mkubwa wa Somaliland Hargeisa, pamoja na mji mkuu wa Somalia Mogadishu pamoja na miji minne ya majimbo ya Somalia.

    

Related Posts