Dar es Salaam. Wakati ikielezwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi Afrika na ya kimkakati wa kibiashara, Kampuni ya DHL Express imejitolea kuja na ajenda ya kulinda mazingira.
Mkurugenzi wa Kanda wa Nchi za Kusini na Afrika Mashariki wa Kampuni ya DHL Express, Fatima Sullivan amesema hayo jana Jumatano Agosti 12 jijini Dar es Salaam, kwenye meza ya mazungumzo ya maofisa watendaji wakuu wa sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nchi yaliyoandaliwa na kampuni hiyo.
Amesema wataendelea kuziendeleza biashara ndogo na za kati kwa kuzijengea uwezo zaidi na kuhakikisha zinarasimishwa na kufanywa kwa urahisi ndani na nje Tanzania.
“Tuna bidhaa inayojulikana kama SME 360, ambayo tutahakikisha biashara ndogo na za kati na ambazo miongoni mwake kuna za kifedha na taasisi za biashara zinaendeshwa vizuri,” amesema Sullivan.
Hata hivyo, amesema DHL Express, ambayo ndiyo kampuni kubwa zaidi ya usafirishaji duniani, imejitolea kuhakikisha inafanya kazi katika mazingira safi zaidi.
“Ndege zetu zinafanya kazi duniani kote kusafirisha mizigo na hutoa kaboni nyingi. Tunafanya kazi ili kuhakikisha kuwa utoaji wa kaboni unafikia mwisho (sifuri) ifikapo mwaka 2050, “amewaambia maofisa watendaji wakuu kutoka sekta mbalimbali.
Pia, amesema kuna utafiti na majaribio ya aina mbalimbali juu ya ndege za umeme ambazo hazitoi kaboni.
“Ni utafiti wa kina ambao utachukua muda kwa sababu sisi sote tunajua sekta ya usafiri wa anga ni nyeti,”amesema.
Sullivan pia amesisitiza kujitolea kwa DHL kwa ajenda ya kijani ambayo kupitia kwao kampuni itawashirikisha wenyeji kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa.
“Tunapanga kutekeleza miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ambayo itatusaidia kutoa huduma bora zaidi,” amesema Sullivan.
Kuhusu mazingira ya biashara nchini Tanzania, Sullivan amewaambia maofisa watendaji wakuu kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zinazokua kwa kasi kubwa Afrika na mdau muhimu katika kanda, hivyo ni nchi ya kimkakati wa kibiashara.
Ameonyesha umuhimu wa biashara ndogo na za kati na nafasi yake katika biashara ya DHL.
Meneja wa DHL nchini Tanzania, Humphrey Pule amesema walifurahi sana kuwa mwenyeji wa meza ya mazungumzo ya wakati wa kifungua kinywa.
Amesema kampuni hiyo imewapa wadau maarifa mengi kuhusu mazingira ya biashara na jinsi gani kwa pamoja wanaweza kutatua baadhi ya changamoto zinazoathiri biashara nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na miundombinu na taratibu za udhibiti.
“Tunatazamia kuwa mwenyeji wa mikutano mingi zaidi kwa siku zijazo kwani ni muhimu kwa biashara,” amesema Pule.
Tukio hilo liliwaleta pamoja maofisa watendaji wakuu na baadhi ya wabia wa DHL ambao wanafanya kazi ndani na nje ya Tanzania.