Tawido yalia na Dar matukio ya ukatili

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umedaiwa kurekodi matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kutokana na kesi walizopokea Shirika la Tanzania Women Initiatives for Development Organization (Tawido).

Takwimu hizo zimetolewa leo agosti 21 ,2024 na mkurugenzi wa shirika hilo, Sophia Lugilahe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia katika ofisi zao zilizopo Mbezi Makonde  jijini Dar es Salaam.

Amesema, Tawido limepokea jumla ya matukio 38,238 kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, huku wanawake wakiongoza kwa idadi kubwa ambayo ni 27,824, wakifuatiwa wanaume 9,352 na watoto 9,038.

Akielezea aina ya ukatili wanaoupitia waathirika hao, walionyanyaswa kingono ni 13,216, kimwili ni 12,243, kisaikolojia 7,403 , kiuchumi 3375 na  watoto 938 kwa kipindi cha 2021 mpaka 2024.

“idadi hii ya matukio ni kwa wale waliofanikiwa kupata namba zetu na kutupigia simu, hapa unaona jinsi gani matukio haya yamekithiri katika jamii”

Aidha, mkurugenzi huyo amesema, matukio ya hivi karibuni ya kuteka watoto ni matokeo ya ukatili unaofanyika bila kutoa taarifa yoyote na matukio hayo ni yale yanayoripotiwa na wasamaria wema katika jamii na wala si wahanga wenyewe.

Pia, Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali itenge bajeti kwaajili yakushughulikia matendo yakikatili yanayoendelea katika jamii.

Naye, Tumainieli Eliasi, mwenyekiti wa shirikisho la bodaboda Kata ya Mbezi juu jijini Dar es Salaam ambaye ni mwanachama wa Tawido amesema kulingana na matukio ya kikatili yanayoendelea amechukua jukumu la kuwaelimisha madereva katika vituo kwa mikutano mbalimbali.

“Bodaboda anabeba kila aina ya abiria hivyo nawahamasisha madereva hao kutoa elimu ya jinsia pale anapokuwa amebeba abiria,”ameeleza

Dereva huyo ameiomba pia serikali kutenga fungu litakalowezesha uhamasishaji wa kutoa elimu kuhusu ukatili katika sehemu mbalimbali kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu mpaka  nyumba za ibada.

Related Posts