THBUB YATOA TAMKO KUHUSU KUPOTEA KWA WATU NCHINI

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Kufuatia matukio ya kupotea kwa watu nchini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imesema inaendelea kufanya chunguzi maalum za matukio hayo kwa lengo la kubaini, pamoja na mambo mengine chanzo na wahusika ili kutoa mapendekezo stahiki.

Hayo yameelezwa leo Agosti 22,2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu matukio hayo na kubainisha mikoa inayohusishwa na chunguzi hizo.

“Chunguzi hizo zinazoendelea kwa sasa zinahusisha mikoa ifuatayo Dar es Salaam, Singida, Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita, Kigoma, Tanga, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma na Rukwa, hatua hii ni mwendelezo wa chunguzi zinazohusu matukio ya kupotea kwa watu ambayo THBUB imekuwa ikiyafanyia kazi katika nyakati tofauti na taarifa zake kufikishwa katika vyombo vinavyohusika”, amesema.

Aidha, amesema katika kufanikisha lengo la taarifa kwa waliyotola na Julai 19,2024 iliyokuwa inaeleza kazi ilizokuwa imetekeleza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 hususan katika eneo la uchunguzi wa malalamiko ya wananchi kuhusu uvunjifu wa haki za binandamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora THBUB ilikuwa imekwishafanya hatua mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa matukio hayo kwa maana ya sehemu yalikotokea na watu waliokuwa wanadaiwa kuhusika.

“Pia tulikuwa tumeandaa mpango kazi wa namna ya kufuatilia matukio hayo kwa kuzingatia mamlaka yake na kuendelea na chunguzi kuhusu matukio hayo”,amesema.

Aidha akizungumzia kuhusu vurugu zilizotolea siku ya jana Mkoani Simiyu zilizosababishwa na madai ya kupotea kwa watoto Jaji Mstaafu Mwaimu amesema wataenda kufanya uchunguzi ili kuweza kulishughulikia suala hilo.

Tume ya haki za binadamu na utawala bora inatekeleza majukumu hayo chini ya ibara ya 130 (1)(b) na (c) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kifungu cha 6 (1)(b) cha sheria ya haki za binadamu na utawala bora sura ya 391.

Related Posts