Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha uwepo wa joto kali na uwezekano wa kuwapo mlipuko wa magonjwa katika kipindi cha mvua za vuli kitakachoanza Oktoba hadi Desemba, 2024.
Mbali na athari hizo, sekta ya kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji wa nchi kavu, majini na angani zinaelezwa zitaathirika na hali hiyo ya hewa, hivyo menejimenti za maafa zimetakiwa kuchukua tahadhari mapema.
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema hayo leo Agosti 22, 2024 alipokuwa akielezea mwelekeo wa mvua za vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2024.
Dk Chang’a amesema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba, 2024 katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba, 2024.
“Uwepo wa La-Nina hafifu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua msimu wa vuli, 2024,” amesema.
La Nina ni hali ya hewa inayotokea kwenye bahari ya Pasifiki ya Kati na Mashariki, ambayo joto la uso wa bahari linapungua kuliko kawaida. Hali hii husababisha mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Mtaalamu wa Hali ya Hewa TMA, Dk Alfred Kondowe amesema utabiri wa mvua za masika walioufanya Machi hadi Mei ulikuwa sahihi kwa asilimia 98.4.
“Hali ya upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama inaweza kujitokeza na kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile vikope, ngozi, kipindupindu, homa ya matumbo, changamoto ya kupumua na magonjwa yanayohusiana na joto kali,” amesema Dk Chang’a.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Dk Chang’a amesema mamlaka husika zinashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari hasi, ikiwa ni pamoja na kuhimiza wananchi kutibu maji kabla ya kunywa, kusafisha matunda, kunywa maji safi, salama na ya kutosha ili kuepuka upungufu wa maji mwilini na kuzingatia usafi wa mwili na mazingira.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Englibert Kayombo amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wametoa mwongozo wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko nchini.
Amesema miongozo inatekelezwa wakati wote akieleza kanda ya ziwa kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na timu ya wataalamu inaendelea kudhibiti.
“Tunashirikiana na TMA wanapotupa taarifa tunazifanyia kazi, hasa kutoa elimu kwa wananchi na kusambaza vidonge vya watu kuweka kwenye maji kuepuka kunywa maji yasiyo salama. Bohari Kuu ya Dawa (MSD) inaendelea na usambazaji wa vifaatiba, hivyo udhibiti wa magonjwa ya mlipuko tunaufanya wakati wote,” amesema.
Dk Chang’a akizungumzia kuhusu sekta ya utalii na wanyamapori, amesema mvua chache itasababisha mwingiliano baina ya jamii na wanyamapori.
“Baadhi ya magonjwa ya wanyamapori kutokana na upungufu wa mvua yanaweza kutokea na kusambaa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa binadamu, mamlaka husika zinashauriwa kuelimisha jamii kuchukua tahadhari kuhusu athari zinazoweza kujitokeza,” amesema.
Kwa upande wa maji, nishati na madini, Dk Chang’a amesema kupungua kwa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kunatarajiwa kujitokeza.
“Hali hii inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali, uzalishaji wa madini (hususan dhahabu kwa wachimbaji wadogo) na nishati ya umeme utokanao na maji unaweza kuathirika.
“Katika sekta ya maji, watumiaji wataathirika kijamii, kiuchumi, na mazingira na kusababisha migogoro kati ya watumiaji wakubwa na wadogo. Hata hivyo, utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya maji, umeme, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi unatarajiwa kuendelea vizuri,” amesema.
Dk Chang’a amesisitiza kuzingatiwa mgawanyo wa maji na matumizi endelevu katika shughuli za kuchakata madini, uzalishaji wa umeme, matumizi viwandani na majumbani na mamlaka zinazohusika na nishati ziwe na mipango madhubuti ya matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati.
Dk Chang’a amesema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za vuli, hususan maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa pwani ya kaskazini.
Amesema hali hiyo inatarajiwa kuathiri ukuaji wa mazao, huku wadudu na magonjwa ya mazao yakitarajiwa kuongezeka katika msimu huo, hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao.
“Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo. Aidha, wanashauriwa kuandaa mashamba kwa wakati, kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame,” amesema.
Dk Chang’a amesema kutokana na upungufu wa malisho na maji, kuna uwezekano wa migogoro kujitokeza baina ya wafugaji na watumiaji wengine.
Amesema shughuli za kibiashara zinazohusisha hali ya hewa zitaathirika kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.
Amesema hiyo ni kutokana na matumizi makubwa ya nishati katika uhifadhi wa mazao tete na bidhaa, akisisitiza sekta binafsi ishirikiane na wataalamu wakiwamo wa hali ya hewa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
“Hatua za kupunguza matawi ya miti ya nguzo na mbao zitekelezwe mara kwa mara. taasisi za benki na bima zinashauriwa kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau ili kujenga ustahimilivu katika biashara,” amesema.
Amesema sekta ya usafirishaji hususan wa ardhini utakuwa na unafuu kutokana na vipindi vya ukavu vinavyotarajiwa.
“Inashauriwa kwa kipindi husika mipango ya uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji ifanyike kwa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa uliohuishwa katika eneo husika,” amesema.
Dk Chang’a ametaja mikoa 13 itakayokumbwa na athari hizo itakayochangiwa na uchache wa vipindi vya mvua vya wastani na chini ya wastani.
“Mikoa ya Pwani ya kaskazini Morogoro, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba, mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa kuanzia wiki ya pili na ya tatu ya Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya Desemba, 2024,” amesema.
Pia mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Kigoma mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.
Dk Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba, 2024 katika mikoa ya Kagera, Geita na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na kutawanyika maeneo mengine wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba, 2024 na zitaisha wiki ya tatu na ya nne ya Desemba, 2024.
“Nyanda za juu kaskazini Mashariki mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu Kaskazini mashariki. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya Oktoba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya Desemba,” amesema.